Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 11Article 556891

Siasa of Saturday, 11 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Gwajima, Jerry Silaa na Polepole wajadiliwa Kamati Kuu CCM

Gwajima, Jerry Silaa na Polepole wajadiliwa Kamati Kuu CCM Gwajima, Jerry Silaa na Polepole wajadiliwa Kamati Kuu CCM

KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekiri kupokea taarifa za wabunge watatu wa chama hicho waliohojiwa hivi karibuni na Kamati ya Maadili ya Uongozi wa Bunge kwa tuhuma mbalimbali.

Aidha, Kamati Kuu ya CCM imeteua majina ya wanachama watakaopeperusha bendera ya chama katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Ushetu na Konde.

Hayo yameelezwa jana jijini hapa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa,Shaka Hamdu Shaka baada ya kumalizika kwa kikao cha kawaida cha Kamati Kuu kilichokutana Ikulu ya Chamwino chini ya Mwenyekiti Rais Samia Suluhu Hassan.

Shaka alisema tayari chama kimepokea taarifa ya wabunge hao watatu, Askofu Josephat Gwajima (Kawe), Humphrey Polepole (Kuteuliwa) na Jerry Silaa (Ukonga), na kinachoendelea ni taratibu za ndani kwa misingi ya Katiba na kanuni.

Hivi karibuni wabunge hao watatu walihojiwa na Kamati ya Maadili ya Uongozi wa CCM bungeni kutokana na kwenda kinyume cha chama hicho. Ilielezwa baada ya kikao hicho kuwa shauri ao limepelekwa kwa Kamati ya Uongozi ya CCM bungeni ambayo Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Awali, Gwajima na Silaa walihojiwa na Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma za kusema uongo na kushusha hadhi na heshima ya Bunge kabla ya Bunge kuazimia adhabu ya kutohudhuria mikutano mwili ya Bunge.

“Chama Cha Mapinduzi kina misingi yake yanayozingatia Katiba na kanuni za chama. Nakiri ni kweli chama kimepokea taarifa ya Kamati ya Wabunge na hatua zinazofuata ni ziko ndani ya chama kulingana na Katiba na kanuni.

“Ninawahakikishia kwamba CCM bado iko imara hasa katika kulinda na kuhakikisha inaendeleza msingi ya kuanzishwa kwake,” Shaka aliwaambia waandishi wa habari.

Aidha, Shaka alisema Kamati Kuu imewapongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kwa jinsi wanavyowaletea maendeleo wananchi na kuridhishwa na kutekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Pia, imempongeza Rais Samia kwa kazi kubwa ya kuisimamia serikali na kuhakikisha imesimama kwenye mstari wake katika kuwatetea, kuwasemea na kuwapigania Watanzania katika kuwaletea maendeleo endelevu.

“Mheshimiwa Rais Samia katika hili ameonesha umahiri, uimara na uthubutu wa kuhakikisha kwamba badala ya kurudi nyuma tunasonga mbele kwa kasi kubwa,” alisema Shaka.

Aliongeza, “Kamati Kuu kwa dhati imempongeza Dk Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi, wote tumeshuhudia akiwa ametoka kwenye ziara ya kutembelea visiwa vya Unguja na Pemba na kuonyesha utayari na kuonyesha kile ambacho tumekiahidi kwa Watanzania.”

Akizungumzia Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Konde na Ushetu, alisema Kamati Kuu imefanya uteuzi ya wagombea, ambao ni Emmanuel Cherehani kwa Jimbo la Ushetu mkoani Shinyanga wakati kwa upande wa Jimbo la Konde kisiwani Pemba, imeteua Mbarig Amor Habib.

Alisema kampeni za CCM kwa Jimbo la Ushetu zitazinduliwa Septemba 25, mwaka huu na Naibu Katibu Mkuu Bara, Christine Mndeme, na Konde zitazinduliwa Septemba 24, na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Dk Abdallah Juma Sadalla.