Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 12Article 585115

Siasa of Wednesday, 12 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Haya ndiyo maisha mapya ya Ndugai Bungeni

Job Ndugai, aliyekuwa  Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania

Bado mjadala kuhusu stahiki ambazo atapata aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai unazidi kupamba moto hasa kuhusu kama anastahili au la.

Ndugai alijiuzulu nafasi hiyo Januari 6, mwaka huu, baada ya kutoa kauli tata kuhusu mikopo ya Serikali kwenye mkutano na umoja wa wasomi wa Kigogo uliofanyika Desemba 26, mwaka jana.

Kauli hiyo ya Ndugai iliyosoa Serikali kukopa nje akilinganisha na alichokiita “kujibanabana na kufanya mambo yetu” ilionekana kupishana na msimamo wa Rais Samia Suluhu Hassan aliyefafanua siku moja baadaye, kuwa Serikali itaendelea kukopo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kupishana kauli kwa viongozi hao wakuu wa mihimili kuliibua mjadala huku baadhi ya viongozi na makada wa CCM wakiwemo wabunge wakijitokeza kumshambulia Ndugai na kumshinikiza ajiuzulu, uamuzi alioufikia Januari 6, mwaka huu.

Kwa kujiuzulu, ni dhahiri si tu enzi zake za ukuu, utukufu na utawala wake bungeni umeisha, bali pia Ndugai atakosa mamlaka makuu ya kisiasa, ikiwemo kuongoza mhimili wa dola na ujumbe wa Kamati Kuu ya CCM aliyokuwa akiingia kwa nafasi yake.

Pia Ndugai kwa sababu hiyo anakosa vitu kadhaa alivyovizoea kwa kipindi cha miaka sita iliyopita ikiwemo kukalia kiti cha Spika, sauti ya mwisho katika mambo ya Bunge na kuuvua ukuu wa mhimili wa dola.

Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria ataendelea kupata haki, stahiki na manufaa kadhaa kwa nafasi aliyoshika, lakini nguvu, mamlaka na ushawishi wa kisiasa vitakuwa vimefika kikomo au kupungua makali.

Japo kwenye siasa mambo yanaweza kubadilika hapo baadaye, kama ambavyo iliwahi kutokea kwa baadhi ya walioachia ngazi baadaye wakaibuka kivingine na kushika nyadhifa kubwa zaidi au kupotea kabisa.

Kiti cha enzi bungeni

Tangu Novemba 17, 2015 hadi Januari 6, 2022 alipojiuzulu, Ndugai ndiye alikuwa kiongozi mkuu wa mhimili wa Bunge akiwa anaketi kwenye kiti cha Spika huku amevaa joho lenye heshima.

Japo alikuwa na uzoefu wa kukikalia kiti hicho tangu akiwa Mwenyekiti wa Bunge wakati wa uspika wa marehemu Samuel Sitta na Naibu Spika chini ya Anne Makinda, ukuu na enzi kamili wa Ndugai bungeni ulianza alipopokea kiti hicho baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Enzi, utukufu na ukuu huo sasa umeisha tangu Januari 6 kwani, kuanzia Februari mosi vikao vya Bunge vitakapoanza, Ndugai ataketi kiti cha nyuma cha mbunge wa Kongwa tofauti na mazoea yake ya miaka sita iliyopita ya kuketi kwenye kiti cha enzi mbele ya Bunge.

Ukuu wa mhimili

Kwa miaka sita iliyopita, Ndugai amekuwa kiongozi na mkuu wa mhimili wa Bunge akiwa ndiye mwenye sauti na kauli ya mwisho wakati na hata nje ya vikao vya chombo hicho.

Mihimili mingine ya dola ni Mahakama unaoongozwa na Jaji Mkuu na Utawala (Serikali) unaoongozwa na Rais, ambaye pia ndiye mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Kwa mujibu wa kanuni, anayekalia kiti cha spika ndiye mwenye mamlaka na uamuzi wa mwisho wa shughuli zote bungeni ikiwemo kuamua kwa busara zake nani aseme, aseme kwa muda gani na nani asizungumza.

Kwa lugha rahisi, kiti cha spika ndicho alfa na omega -- mwanzo na mwisho bungeni na kinachoamuliwa na kiti ndicho kinachofanyika hadi itakapoamuliwa vinginevyo kwa taratibu zingine za kikanuni.

Haya ni mamlaka na enzi ambayo Ndugai atayakosa kwa sababu naye sasa atalazimika kuomba ruhusa ya Spika au anayekikalia kiti cha spika ndipo azungumze bungeni.

Kuketisha, kutoa wabunge ukumbini

Katika matukio na nyakati tofauti, kiti cha Spika akiwemo Ndugai mwenyewe, kimewamuru wabunge kadhaa kuketi chini, kuacha hoja zao, kufuta kauli au kutoka nje ya ukumbi chini ya ulinzi.

Wapo wabunge akiwemo Joseph Mbilinyi aliyekuwa mbunge wa Mbeya Mjini, waliwahi kutolewa bungeni kwa kubebwa mzobemzobe na askari wa Bunge kwa amri ya Ndugai, mamlaka ambayo sasa ameyapoteza.

Kuunda kamati, taratibu za itifaki

Tofauti na alivyozoea kuunda kamati za Bunge, kuteua wenyeviti na wajumbe kwa miaka sita iliyopita, Ndugai naye sasa anamsubiri spika ajaye ampangie kamati atakayohumu kwa namna atakavyoona inafaa.

Miaka sita iliyopita, Ndugai amefaidi masilahi na taratibu za kiitifaki ikiwemo msafara wake kuongozwa na ving’ora, ulinzi wa saa 24 kazini, nyumbani na mitaani na marupurupu kadhaa ya nafasi ya spika, mambo ambayo yameondoka au yatapungua kwa kiwango kikubwa.

Katika matukio kadhaa ya kitaifa yanayomhusisha Rais, imezoeleka kuwaona Spika, Jaji Mkuu na viongozi wengine wa juu wakiketi sambamba, fursa ambayo Ndugai ataikosa baada ya kujiuzulu.

Kwa maana hiyo, Ndugai atakuwa akiomba nafasi ya kuchangia na kuuliza swali, kufuata kanuni na taratibu zote ikiwemo kusimama pindi spika, naibu wake au wenyeviti wanapoingia bungeni.

Awali, wabunge walikuwa wakisimama kutoa heshima pindi Ndugai anapoingia ukumbini akisindikizwa na maofisa wa Bunge.

Wabunge watakuwa na fursa ya kuomba muongozo ama kumpa taarifa Ndugai pindi anapochangia mjadala.

Kwa nafasi yake ya awali, Ndugai alikuwa na fursa ya kuwakilisha Bunge katika vikao, taasisi na vyombo vya kimataifa, nafasi ambayo sasa hatakuwa nayo.

Maslahi ya Ndugai kisheria

Licha ya kuachia ngazi kwenye wadhifa huo, lakini kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Utumishi wa kisiasa ya 1999, kiongozi anayeacha kushikilia nafasi ya Spika wa Bunge, atakuwa na haki ya kupata mafao yafuatayo baada ya kuacha kushikilia nafasi hiyo;

a) Kiinua mgongo cha asilimia 50 ya fedha zote alizowahi kuzipokea kama mshahara wakati akiwa Spika.

b) Pensheni kwa mwaka itakayolipwa kila mwezi ambayo ni sawa na asilimia 80 ya mshahara anaolipwa Spika aliyepo madarakani.

c) Posho ya kufungasha mizigo ambayo ni sawa na mishahara ya miezi 24.

d) Gari moja atakalonunuliwa na Serikali.

e) Dereva atakayelipwa na Serikali.

f) Pasi ya kibalozi kwa ajili yake na mke au mume wake.

g) Lita 70 za mafuta kwa wiki.

h) Posho ya kukarabati gari ambayo ni sawa na asilimia 40 ya posho ya mafuta kwa mwezi.

Akiijadili sheria hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alisema Ndugai anakwenda kuvuna utajiri.

“Mnaposhangilia hapa, Spika Ndugai anachekelea kuelekea benki, wakati ninyi mnashangilia kuwa ametoka, anakwenda kupata pensheni nono. Pensheni hii yote ni mpaka kufa kwake, kwa kazi gani kubwa aliyofanyia Taifa? Hayo yote yanatakiwa kujadiliwa kwenye Katiba mpya,” alisema Lissu.

Hata hivyo, Wakili John Seka alisema mafao hayo yako sawa kwa lengo la kulinda hadhi ya viongozi wa juu wa Serikali.

“Sioni ukandamizaji wa hiyo sheria,” alisema Seka huku akitoa mfano wa Rais.

“Huyo ni Rais, anapoachia madaraka yake lazima aishi kama Rais. Wapo kama Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Majaji na wengineo. Wanapokuwa madarakani hawatakiwi waone njaa, wasije wakatumia madaraka yao vibaya kujitajirisha,” alisema.

Cheo ni koti la kuazima

Akizungumzia kilichotokea, Edwin Soko, mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa alimshauri Ndugai na wanasiasa wengine kukubaliana na ukweli kwamba, vyeo vya kisiasa ni sawa na koti la kuazima linaloweza kuondoka wakati wowote mwenye nayo akiamua.

“Vyeo vya kisiasa hupatikana kwa kupigiwa kura au kuteuliwa na zinaweza kuondoka wakati wowote bila kutarajia kama ilivyotokea kwa Ndugai, ambaye kauli yake moja tu kuhusu mikopo ya Serikali imemlazimu kujiuzulu”.