Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 08Article 584083

Siasa of Saturday, 8 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Hili hapa tamko la UVCCM kwa watakaomhujumu Rais Samia

Katibu wa UVCCM, Kenani Kiongosi, Katibu wa UVCCM, Kenani Kiongosi,

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umeahidi kumlinda na kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika shughuli zake zote huku ukisisitiza kuwa hautavumilia uvunjifu wa heshima utakaofanywa na wasaidizi wake kwa lengo la kumhujumu.

Katibu wa UVCCM, Kenani Kiongosi, amesema hayo katika risala yake kwa Rais Samia jana mjini Pemba aliposhiriki maandamano ya maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoshirikisha watu zaidi ya 700 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar waliotembea umbali wa kilometa zaidi ya 100.

Kiongosi amesema matembezi hayo yanaenzi Mapinduzi ya Zanzibar na yalilenga kuacha alama kama za watangulizi wao.

“Vijana tumeahidi kukusaidia na kukulinda, hatutasita kuwasema watendaji wako wanaokusaidia ambao watakwenda kinyume na wewe kiutendaji na wasijaribu kukuhujumu,” alisema Kiongosi.

Alimpongeza Rais kwa hatua ya kupanua Diplomasia ya Uchumi na kupata Sh trilioni 1.3 ambazo ni mkopo zilizotumika kufanya kazi za maendeleo kwa wananchi na kuacha alama.

Kiongosi alieleza kuwa matembezi hayo yana malengo matatu ambayo ni kuhamasisha vijana kufanya kazi kwa bidii na nidhamu, kupinga vitendo vya rushwa, ubadhirifu na uzembe kazini na kupinga udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto.

Awali, Rais Samia alisema pamoja na changamoto ya janga la corona lililosababisha nafasi za ajira kupungua kutokana na baadhi ya viwanda na taasisi mbalimbali kufungwa kuepusha maambukizi, lakini serikali ya Tanzania imetoa fursa mbalimbali za ajira.

Alisema fursa hizo zimewezesha kutoa ajira zaidi ya 14,000 kwa kipindi cha miezi tisa tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani na ajira nyingi zimeenda kwa vijana na kwamba fursa zaidi zitaendelea kutafutwa.

“Nitoe wito tu kwa vijana kuchangamkia fursa na pia nimpongeze Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa kutenga Sh bilioni 85.4 kwa ajili ya vijana, hivyo changamkieni hizo kwa kuandika maandiko ya miradi yenye tija na hasa tumieni fursa ya mabadiliko ya tabia nchi kubuni miradi ya kuhifadhi misitu,” alisema Rais Samia.