Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 10Article 542104

xxxxxxxxxxx of Thursday, 10 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Hivi ndivyo Pato la Taifa lilivyokua 

SERIKALI imesema licha ya mlipuko wa UVIKO-19 ulioathiri uchumi wa nchi, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizokuwa na ukuaji chanya wa uchumi kwa mwaka 2020 huku pato la Taifa likikua kwa kwa asilimia 4.8.

Hayo yameelezwa bungeni leo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati wa kuwasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2021/22.

Alisema Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.8 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2019.

Dk Mwigulu alisema ukuaji chanya ulitokana na hatua ya Serikali ya kuruhusu shughuli za kiuchumi na kijamii kuendelea na wakati huohuo wananchi wakisisitizwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.

"Aidha, kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi nchini kulichangiwa na athari za UVIKO-19 katika nchi washirika wa kibiashara pamoja na mafuriko yaliyosababisha uharibifu wa miundombinu ya usafirishaji na kuchelewesha utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo."

Dk Mwihulu alisema kuwa athari za janga la UVIKO-19 zilijitokeza zaidi katika shughuli za kiuchumi za malazi, huduma ya chakula pamoja na sanaa na burudani ambazo zilikuwa na ukuaji hasi kwa mwaka 2020.

Akizungumzia sekta zilizokua kwa viwango vya juu kwa mwaka 2020 ni pamoja na Sekta ya Ujenzi (asilimia 9.1), Habari na Mawasiliano (asilimia 8.4), Uchukuzi na Uhifadhi wa Mizigo (asilimia 8.4), Huduma zinazohusiana na Utawala (asilimia 7.8), shughuli za kitaalamu, sayansi na ufundi (asilimia 7.3), Madini na Mawe(asilimia 6.7) na Afya na Huduma za Jamii (asilimia 6.5).

Dk Mwigulu alisema Pato ghafi la Taifa lililozalishwa nchini lilikuwa Sh trilioni 148.5 mwaka 2020, ikilinganishwa na shilingi trilioni 139.6 mwaka 2019.

Aidha, mwaka 2020, Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa na watu milioni 55.9, ikilinganishwa na watu milioni 54.2 mwaka 2019.

Hivyo, Wastani wa Pato kwa Mtu lilikadiriwa kufikia shilingi 2,653,790, sawa na dola za Marekani 1,151.0 mwaka 2020 ikilinganishwa na sh. 2,573,324, sawa na dola za Marekani 1,118.9 mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.1.

Mwenendo wa Bei

Dk Mwigulu alisema kuwa mfumuko wa bei umeendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ambapo ulipungua kutoka wastani wa asilimia 3.4 mwaka 2019 hadi asilimia 3.3 mwaka 2020.

Alisema mfumuko wa bei umebaki katika wigo wa asilimia 3.3 Mei 2021.

" Mwenendo wa mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu kutokana na upatikanaji wa chakula cha kutosha, kushuka kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia, utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani na sarafu nyingine duniani na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti."

Alisema Serikali kupitia Benki Kuu imeendelea kusimamia utekelezaji wa sera ya fedha ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi ambayo imesaidia kupunguza baadhi ya viwango vya riba katika masoko ya fedha hususan riba za mikopo.

Alisema wastani wa riba za mikopo ya benki kwa ujumla katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021 ulipungua hadi asilimia 16.58, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 16.91 katika kipindi kama hicho mwaka 2020, na riba za mikopo ya kipindi cha mwaka mmoja zilipungua na kufikia wastani wa asilimia 16.05 kutoka asilimia 16.37.

Aidha, Dk Mwigulu wastani wa riba za amana kwa ujumla ulikuwa asilimia 6.95 katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.69 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Alisema Riba za amana za kipindi cha mwaka mmoja ziliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 8.77 katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021 ikilinganishwa na asilimia 8.01 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Ukuaji uchumi

Dk Mwigulu alisema taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili 2021 inaonesha kuwa, mwaka 2020, dunia ilikuwa na mdororo wa uchumi kwa kupata ukuaji hasi wa asilimia 3.3 ikilinganishwa na ukuaji chanya wa asilimia 2.8 mwaka 2019.

Alisema ukuaji hasi ulisababishwa na kupungua kwa shughuli za kiuchumi duniani hususan, biashara, usafirishaji na utalii kutokana na mlipuko wa UVIKO-19.

Hata hivyo, alieleza uchumi wa dunia unatarajiwa kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 6.0 mwaka 2021 na asilimia 4.4 mwaka 2022.

"Hii inatokana na matarajio ya kurejea kwa shughuli za kiuchumi kutokana na kuendelea kusambazwa kwa chanjo ya UVIKO-19 na hatua za kuinua chumi zinazochukuliwa na nchi mbalimbali,"alisema.

Mwenendo wa Mikopo kwa Sekta Binafsi

Dk Mwigulu alisema mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia 4.8 katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 5.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Alisema ukuaji mdogo wa mikopo kwa sekta binafsi ulitokana na athari za UVIKO - 19 kwenye shughuli za kiuchumi nchini.

" Sehemu kubwa ya mikopo ilielekezwa katika shughuli binafsi ambazo zilipata asilimia 35.8 ya mikopo yote, ikifuatiwa na shughuli za biashara asilimia 15.7, uzalishaji viwandani asilimia 10.1 na kilimo asilimia 8.0."

Akiba ya Fedha za Kigeni

Alisema kuwa akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.

" Hadi Aprili 2021, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Marekani bilioni 4.97 ambayo inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takribani miezi 5.8."

Alisema kiwango hicho ni zaidi ya lengo la nchi la kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa muda wa miezi 4.0 na ni zaidi ya lengo la miezi 4.5 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Thamani ya Shilingi

Alieleza thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani imeendelea kuwa tulivu ambapo dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,298.5 Aprili 2021, ikilinganishwa na wastani wa shilingi 2,291.3 Aprili 2020.

Alisema Utulivu wa shilingi umetokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika usimamizi wa Sera za Fedha na Bajeti, kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nje ya nchi pamoja na mwenendo chanya wa baadhi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Vilevile, hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania katika kusimamia misingi ya uwazi katika ununuzi na uuzaji wa fedha za kigeni nchini zimechangia thamani ya shilingi dhidi ya sarafu nyingine kubwa duniani kuwa tulivu.

Deni la Serikali

Dk Mwigulu alisema hadi Aprili 2021, deni la Serikali lilikuwa Sh trilioni 60.9, ikilinganishwa na Sh trilioni 55.5 kipindi kama hicho mwaka 2020. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni Sh trilioni 43.7 na deni la ndani ni Sh trilioni 17.3.

Alisema ongezeko hilo lilitokana na kupokelewa kwa fedha za mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

" Taarifa ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2020 inaonesha kuwa deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu kwa kuzingatia ukomo wa viashiria vyote vinavyokubalika kimataifa."

Join our Newsletter