Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 22Article 543790

Habari Kuu of Tuesday, 22 June 2021

Chanzo: ippmedia.com

Hoja 6 zinazohitaji majibu ya Mwigulu

Hoja 6 zinazohitaji majibu ya Mwigulu Hoja 6 zinazohitaji majibu ya Mwigulu

Mjadala wa siku saba wa bunge ulitawaliwa na hoja nyingi na kubwa ambazo zilichukua sehemu kubwa ya mjadala ni kodi za laini za simu, kodi ya miamala, ulipaji kodi ya majengo kwa kutumia Luku za umeme na kodi kwenye mafuta.

Nyingine ni upigaji wa fedha kupitia stempu za bidhaa, kupanda kwa leseni na wafanyabiashara wa maduka ya kubadilishia fedha walionyang’anywa fedha zao.

Wabunge walitaka ufafanuzi wa serikali kwenye nyumba za wapangaji, nyumba moja yenye Luku zaidi ya moja na nyumba za udongo zilizoezekwa kwa nyasi zilizopo vijijini.

Aidha, walitaka ufafanuzi wa namna kodi ya miamala ya simu na laini za simu zitakavyotozwa, huku kukiwa na hofu ya wananchi wengi kuumia.

Wengine walipongeza kuwa kuna ubunifu katika kutafuta kodi kwa kuwa sasa kodi ya majengo itapatikana kirahisi kupitia malipo ya umeme.

Mapendekezo ya bajeti hiyo ni kutoza kodi ya simu ya Sh. 10 hadi Sh. 200 kila siku kwa kila mwenye laini ya simu, na iwapo itapita itaanza kutekelezwa Julai mosi, mwaka huu.

Nyingine ni kutoza kodi ya Sh. 10 hadi 10,000 kwa mwezi kwa kila muamala wa simu utakaofanywa na watumiaji.

Aidha, imependekeza kutozwa kodi ya majengo ya Sh.1,000 kila mwezi kwa nyumba za kawaida na Sh. 5,000 kwa ghorofa.

Baadhi ya wabunge waliochangia hoja hiyo ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum CCM, Juliana Shonza, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Dk. Charles Kimei, Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango.

KODI YA MAJENGO

Wabunge hao walisema ni vyema serikali ikafafanua kwa kina kodi ya majengo italipwa na nani kwa kuwa zipo nyumba zinakaliwa na wapangaji jambo ambalo huenda wakabeba mzigo mzito.

“Sheria ya majengo ya awali inasema kwamba suala la kulipa kodi ya majengo ni la mwenye nyumba na siyo la mpangaji.

“Kwa hiyo kwenye agizo hili nimwombe sana waziri atakaposimama hapa atuambie serikali imejipangaje, ina mkakati gani ili kuondoa sintofahamu kati ya mwenye nyumba na mpangaji.

“Waziri utuambie kwa wazee wenye msamaha itakuwaje, na kuna zile nyumba ambazo unakuta ni nyumba moja lakini kila mtu ana Luku yake utaratibu uko vipi, pia kuna maeneo ambayo yalikuwa nje ya wigo wa kodi ambayo ilikuwa haiwagusi, je, serikali imejipangaje kuhakikisha wakati wa kuikusanya haileti mgongano?” alisema.

“Waziri ukija hapa ni vizuri ukafafanua kuhusu hii kodi kwa kuwa italeta mikanganyiko kwa wananchi ikiachwa hivi ilivyo,” alisema Kilango.

KADI LAINI ZA SIMU

Baadhi ya wabunge waliochangia hoja hiyo walitaka fedha zitakazotokana na tozo hizo ziwekwe kwenye mfuko maalum, ili zikatekeleze mambo yaliyokusudiwa badala ya kuingia serikalini na kupangiwa shughuli nyingine.

Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, ambaye aliibua hoja ya kodi hiyo, alisema wanaotoa maneno ya kashfa na matusi dhidi ya viongozi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu suala hilo wajue wanalipa kodi kwa kutuma ujumbe huo.

Aidha, Kamati ya Bajeti walisema ubunifu wa kodi ya majengo ni mzuri ila unakwenda kinyume cha sheria ya kodi ya majengo ambayo inaangalia majengo yaliyoko maeneo yanayotakiwa kulipiwa kodi.

“Mapendekezo haya yanachukulia nyumba zote zenye umeme hata zile ambazo ziko vijijini, lakini hazipo kwenye maeneo ambayo kwa mujibu wa sheria hazina sifa ya kutozwa kodi,” alisema Sillo Baran.

Pia alisema mapendekezo hayo hayatoi msamaha kwa taasisi za umma na majengo mengine ya umma ambayo yanatumia umeme lakini kwa mujibu wa sheria yamesamehewa.

“Kuweka kiwango hiki kwa nyumba zilizoko mjini na vijijini ni kuwaumiza wananchi ambao wanaishi vijijini. Kamati inashauri ubunifu uende sambamba na tathmini ya nyumba na kutumia Luku kwa namba ya mlipa kodi na kila Luku itozwe kulingana na nyumba ambayo Luku hiyo ipo,” alisema.

“Utaratibu uwekwe kwa majengo ya maghorofa ambayo yana mkazi zaidi ya mmoja. Hatua hii italeta mapato zaidi kuliko utaratibu huu unaopendekezwa.

KODI YA MAFUTA

Mbunge wa  Kaliua, Aloyce Kwezi na Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangila, walipendekeza kampuni za simu kuchangia kiasi kiasi cha Sh.1,000 kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa sababu barabara za vijijini ndiyo mishipa ya uchumi.

Baadhi ya wabunge walisema hoja siyo tozo hizo bali ni mzigo utakaokuwa unabebwa na kila lita ya mafuta na kuchangia mfumuko wa bei sekta ya usafirishaji na bidhaa.

Pia walishauri kiwango cha Sh. 100 iliyotengwa kwenye mafuta kwa ajili ya TARURA ipelekwe kwa wakati badala ya fedha hizo kupelekwa miezi sita au mwaka au siku za mwisho za kumalizia bajeti.

Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage na Mbunge wa Jimbo la Ndanda (CCM), Cecil Mwambe, walisema kuwa barabara hizo zinatumia fedha nyingi za wananchi na nyingi hazipitiki na nyingine zimekosa mifereji.

Walitaka  kufahamu fedha iliyokusanywa kwa ajili ya miradi ya barabara na maji kwa awamu iliyopita mpaka sasa imekwenda kiasi gani na chenji iliyobaki itapatikana lini.

MADUKA YA KUBADILISHIA FEDHA

Mbunge wa Arusha Mjini, Gambo, alitaka ufafanuzi wa fedha zilizochukuliwa kwenye maduka ya kubadilishia fedha, magari, hati za vyumba na viwanja kwa wafanyabiashara jijini Arusha pamoja na kupanda kwa leseni ya duka hilo kutoka Sh. milioni 300 hadi bilioni moja.

UPIGAJI

Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee, aliitaka serikali kuja na majibu ni lini itavunja mkataba wa uwekaji wa stempu za kielektroniki kwenye bidhaa mbalimbali, kati yake na Kampuni ya Societe Industrielle de Produits Alimentaire (SICPA) ya Uswisi, yenye ubia na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).