Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 26Article 553789

Habari Kuu of Thursday, 26 August 2021

Chanzo: Nipashe

ICU ya Hospitali ya Moyo "JKCI" yazidiwa wagonjwa

ICU ya Hospitali ya Moyo ICU ya Hospitali ya Moyo "JKCI" yazidiwa wagonjwa

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohammed Janab, amesema janga la corona limesababisha vyumba vyao vya Uangalizi Maalum (ICU) kujaa wagonjwa na kushauri wananchi wachanje badala ya kusubiri wafikishwe hospitali wakiwa na magonjwa zaidi ya moja.

Prof. Janab alitoa ushauri huo juzi jioni wakati akitoa elimu ya chanjo na athari zitokanazo na corona kwa wafanyakazi wa shule binafsi ya International School of Tanganyika (IST) iliyoko Upanga jijini Dar es Salaam na baada ya mafunzo hayo, utolewaji wa chanjo kwa hiari ulifanyika shuleni huko.

Akijibu swali la mmoja wa wafanyakazi wa shule hiyo aliyetaka kujua muda wa kutumia dawa kwa mtu mwenye shinikizo la damu endapo akiamua kuchanjwa, Prof. Janab alisema mtu huyo anaweza kuchanja na kuendelea na dozi yake.

Prof. Janab alifafanua kuwa mtu mwenye tatizo la shinikizo la damu, atapata kiharusi ikiwa ataacha kutumia dawa.

"Dawa za shinikizo la damu haziachwi hata dakika moja, shinikizo la damu linaharibu mishipa ya damu, corona inaharibu mishipa ya damu, ninatamani upate muda hata kesho (jana) upite JKCI nikuonyeshe namna ICU zilivyojaa.

"Uje uone watu wanavyoteseka ICU zetu zote hazina nafasi kwa sababu kuna wagonjwa wa COVID-19, ninakupa elimu leo, uamuzi wa mwisho ni wako kuchanja au kutochanja," alisema.

Prof. Janab aliwataka wafanyakazi hao wajiulize wapate corona huku tayari wana maradhi mengine mwilini yanayowasumbua au wajikinge na janga hilo.

"Kipi kirahisi upate corona na shinikizo la damu? Au uje ukiwa na ugonjwa wako wa shinikizo la damu au mwingine tukutibie?

"Nilikuwapo wimbi la kwanza, wimbi la pili, wimbi la tatu sitaki kukumbushia watu waliopoteza maisha, sio kupinga, ni maisha ya watu yanapotea, hatujawahi kupata vifo vingi namna hii, ni uamuzi wa kila mmoja wetu," alisema.

Aliwaondoa hofu wale wanaohofia chanjo kwa kuwaeleza kuwa chanjo zilizopitishwa ni salama.

"Kama mnaniamini mimi, mnaniletea ndugu zenu au ninyi wenyewe, ninafanya upasuaji mkubwa wa moyo, tunausimamisha kwa saa nne au sita halafu ninaupiga umeme uanze tena kufanya kazi, ninaomba mtuamini kwenye hili la chanjo tunachowaeleza," Prof. Janab alisema.

Pia alisema matatizo yaliyopo duniani kwa sasa mahitaji ya chanjo ni makubwa kuliko uzalishaji ndiyo maana nchi zilizoendelea wamelipia huduma hiyo hadi mwakani.

Prof. Janab alitaja takwimu za watu waliojitokeza kuchanjwa katika kituo cha kutolea chanjo kilichoko JKCI na kueleza kuwa hadi siku hiyo, walikuwa zaidi ya 3,500 na kwamba hakuna aliyerudi na kusema amepata matatizo baada ya huduma hiyo.

"Kwa miaka karibu miwili tulichojifunza hautakiwi (corona) ikukute na kitu chochote, haitaki watu wazima, wengi waliofariki ni hao wenye matatizo mengine, ndiyo maana kwa yule mwenye kisukari, shinikizo la damu, figo, saratani, chanjo zilivyokuja tulisema wawe mstari wa mbele kwa sababu ukikukuta na chochote katika hivyo kwa lugha ya mtaani (virusi) vinapata kichaa," alisema.

Mkurugenzi wa IST, Mark Hardeman, alisema shule hiyo imeamua kumwita mtaalamu huyo kutoa elimu ya corona na chanjo kwa wafanyakazi wake baada ya kuridhika na juhudi za Serikali ya Tanzania katika kupambana na janga hilo kwa kuhamamsisha wananchi wakachanje.

"Tumeamua kuwa sehemu ya mapambano hayo kwa kuwawezesha wafanyakazi wetu kupata mafunzo dhidi ya corona na chanjo zinazotolewa ili na wao waamue kuchanja kwa hiari yao," alisema.

Hardeman alisema wana wafanyakazi takribani 260 ambao anaamini elimu iliyotolewa kwao itawawezesha kutambua umuhimu wa kujilinda wao wenyewe na jamii kwa ujumla.

Nipashe ilishuhudia baada elimu hiyo idadi kubwa ya wafanyakazi walioitikia wito wa serikali kuchanja kwa hiari shuleni huko.