Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 27Article 540085

Habari Kuu of Thursday, 27 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

IGP Sirro: Kinondoni kinara wa uhalifu nchini

IGP Sirro: Kinondoni kinara wa uhalifu nchini IGP Sirro: Kinondoni kinara wa uhalifu nchini

MKUU wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amesema Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni unaongoza kwa uhalifu nchini.

IGP Sirro alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na wenyekiti wa serikali za mitaa, watendaji kata na watendaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi vya mkoa huo wa kipolisi.

Aliwataka watendaji hao watimize wajibu wao kwa kuimarisha usalama.

Alisema Kinondoni kuna matukio mengi ya uporaji, kuvunja kwa kutumia nguvu na uporaji kwa kutumia pikipiki, lakini uhalifu mwingine mkubwa wa kutumia silaha za moto umepungua.

Alitoa wiki moja kwa watendaji hao kwa kushirikiana na wenzao wakomeshe uhalifu na akatoa mwito kwa mgambo waache kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tegeta, Mohamed Mawala alisema wataendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia uzalendo, taratibu na kanuni.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mlalakuwa, Suleiman Masare aliahidi kutoa pikipiki mpya kwa Kituo cha Polisi Chuo Kikuu itakayosaidia kurahisisha utoaji wa huduma za kipolisi.

Kabla ya kikao hicho, IGP Sirro alifanya kikao kazi na maofisa na askari wa jeshi hilo akawataka waendelee kutimiza wajibu wao na kuwachukulia hatua wanaojihusisha na uhalifu.

Juzi Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu mkoani humo walianzisha kampeni kudhibiti ujambazi na kuwataka majambazi wasalimishe silaha kwa kuwa hawatakuwa na mzaha

ikikutana nao.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Camillius Wambura katika taarifa yake alieleza kuwa Machi 18 mwaka huu saa 8:00 usiku Polisi walikamata watu watano wakituhumiwa kwa ujambazi.

Alieleza kuwa walikuwa wamekamata watuhumiwa 20 wa makosa mbalimbali.

Wakati huohuo, Sifa Lubasi anaripoti kutoka Dodoma kuwa Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limeanza msako wa mtaa kwa mtaa na kata kwa kata ili kuwakamata wanaojihusisha na uhalifu.

Kamanda wa Polisi

wa Mkoa, Giles Muroto amewataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wajisalimishe, na msako huo pia utahusisha makosa ya usalama barabarani.

“Katika msako huu hatutamuonea mtu, anayetaka kuishi Dodoma awe na kazi halali ya kumuingizia kipato,” alisema Kamanda Muroto alipozungumza na waandishi wa habari.

Alisema Polisi limekamata watuhumiwa 49 wa makosa mbalimbali na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.

Alisema watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa ya mauaji na

kukutwa na silaha kinyume cha sheria, kucheza kamari, unyang’anyi wa kutumia pikipiki, dawa za kulevya, kupatikana na pombe haramu ya moshi (gongo) na kupatikana na mali za wizi,

Alisema msako huo utakuwa endelevu dhidi ya uhalifu wa aina yoyote katika mkoa wa Dodoma na wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wazisalimishe .

“Kama mtu anakuja Dodoma kufanya uhalifu hatakuwa salama, kuna kijana mmoja tumemkamata ni mlemavu wa miguu na anauza bangi na ukimuhoji anasema anafanya biashara ili kusaidia familia,” alisema.

Join our Newsletter