Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 25Article 553606

Habari Kuu of Wednesday, 25 August 2021

Chanzo: www.mwananchi.co.tz

IGP Sirro amuhakikishia Rais Samia usalama wa nchi

IGP Sirro amuhakikishia Rais Samia usalama wa nchi IGP Sirro amuhakikishia Rais Samia usalama wa nchi

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro amesema hali ya usalama nchini inaendelea kuimarika huku matukio ya makosa ya jinai yakipungua.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 25, 2021 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha maofisa wa polisi kinachofanyika jijini Dar es Salaam amesema takwimu zinaonyesha makosa ya jinai yanazidi kupungua.

Ameeleza katika kipindi cha Julai 2020 hadi Juni 2021 makosa yaliyoripotiwa vituo vya polisi yalikuwa 49, 508 ikilinganishwa na makosa 56, 397 kipindi kama hicho 2019/2020.

IGP Sirro amesema kwa idadi hiyo inaonyesha kuna upungufu wa makosa 6859 ambayo ni sawa na asilimia 12.

Soma zaidi: Zaidi ya askari 24,000 wapandishwa vyeo tangu Rais Samia aingie madarakani

Kwa upande wa makosa ya barabarani amesema takwimu zinaonyesha yamepungua kwa asilimia 31.2 na kukiri kuwepo kwa uhalifu unaofanywa na wanaoingia kutoka nchi jirani.

“ Kuhusu uhalifu bado tunao na bado kuna tatizo la Msumbiji lakini tunakwenda vizuri operesheni zinaendelea, wanaoingia humu ndani tunawashughulikia."

“Mikakati iliyopo kupambana na uhalifu ni mingi kubwa ikiwa ni kutoa elimu, kupunguza msongamano wa watu kwenye vituo vya polisi na magerezani,” amesema Sirro.