Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 11Article 542170

xxxxxxxxxxx of Friday, 11 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Idadi ya watu Tanzania Bara yafikia milioni 55.9

IDADI ya watu Tanzania Bara imefikia milioni 55.9 hadi kufikia mwaka jana, kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Akiwasilisha Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2021/2022 bungeni jijini Dodoma jana, Dk Mwigulu alisema idadi ya watu nchini imeendelea kuongezeka kwa wastani wa asilimia 3.1 kwa miaka miwili mfululizo mwaka 2019 na mwaka 2020.

“Makadirio ya idadi ya watu ya mwaka 2020 yanaonesha kuwa idadi ya watu Tanzania Bara imeongezeka kutoka watu 54,265,158 mwaka 2019 hadi watu 55,966,030 mwaka 2020. Kati ya watu hao, wanawake ni 28,550,590 sawa na asilimia 51.0 na wanaume ni 27,415,440 sawa na asilimia 49.0,” alisema Dk Mwigulu.

Akaongeza: “Ongezeko hili ni mtaji mkubwa kwa nchi katika shughuli mbalimbali za uzalishaji katika sekta zote za huduma na uzalishaji. Serikali imeendelea kuweka mikakati na sera madhubuti za kuboresha huduma za kijamii kuendana na mahitaji ya ongezeko la idadi ya watu.”

Alisema serikali imechukua hatua kupunguza umasikini ikijumuisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi kwa kuongeza ujenzi wa majengo ya zahanati na vituo vya afya, ujenzi wa hospitali za halmashauri, kuongeza watalaamu wa afya, dawa na vifaa tiba; utoaji wa elimu msingi bila ada; utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi; utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi; na usambazaji wa umeme mijini na vijijini.

“Hatua hizo zimechangia kuongezeka kwa pato la wastani la kila mtu (GNI per-Capital) na kupungua kwa umaskini. Mathalani, umaskini wa mahitaji ya msingi umepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18. Umaskini wa chakula umepungua kutoka asilimia 9.7 mwaka 2011/12 hadi asilimia 8.0 mwaka 2017/18.”

“Aidha, makadirio ya mwenendo wa umaskini yaliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Umaskini Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka (REPOA) yalibaini kuwa, umaskini unapungua kwa wastani wa asilimia 0.23 kwa mwaka. Hivyo, umaskini umepungua kutoka asilimia 26.4 mwaka 2018 hadi asilimia 25.7 mwaka 2020,” alifafanua.

Alisema matokeo yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za maendeleo yamewezesha mabadiliko chanya katika viashiria vya maendeleo ya watu.

Aliyataja kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa wastani wa umri wa kuishi kutoka miaka 62 (2015/16) hadi miaka 66 (2019/20) na makadirio ya wastani wa miaka 66.6 mwaka 2021; kuongezeka kwa idadi ya Watanzania wenye bima ya afya kutoka asilimia 27 (2016/17) hadi asilimia 34 (2018/19); kupungua kwa idadi ya vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kutoka 432 (2015/16) hadi 321 (2018/19) kwa kila vizazi hai 100,000; vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 67 (2015/16) hadi 50 (2019/20) kwa vizazi hai 1,000.

Mengine ni vifo vinavyotokana na malaria kwa rika zote kupungua kwa asilimia 67 kutoka vifo 6,311 mwaka 2015 hadi 2,079 mwaka 2019.

Kati ya vifo 2,079 vya malaria vilivyotokea mwaka 2019, vifo vya watoto wa umri chini ya miaka mitano, vilikuwa 957 sawa na asilimia 46 ya vifo vyote vitokanavyo na malaria.

Aidha, alisema hali ya upatikanaji wa maji vijijini imeongezeka kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi asilimia 72.3 mwaka 2020 na mijini imeongezeka kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 85 mwaka 2020 na kuongezeka kwa kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya msingi kutoka asilimia 110.3 mwaka 2019 hadi asilimia 110.6 mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Dk mwigulu, pia idadi ya vijiji vilivyounganishwa na umeme imeongezeka kutoka vijiji 7,127 mwaka 2019 hadi vijiji 10,312 mwezi Machi 2021; na idadi ya kaya zilizounganishwa na umeme zimeongezeka kutoka asilimia 32.6 mwaka 2016/17 hadi asilimia 39.9 mwaka 2019/20.

“Ongezeko hilo linaongozwa na maeneo ya vijijini ambapo kaya zilizounganishwa na umeme zimeongezeka kutoka asilimia 16.9 hadi asilimia 24.3 na maeneo ya mijini idadi ya kaya zimeongezeka kutoka asilimia 65.3 hadi asilimia 72.9 kwa kipindi hicho,” alibainisha Dk Mwigulu.

Join our Newsletter