Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 07Article 541495

Habari Kuu of Monday, 7 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ifikapo 2026, mahakama zitakuwepo kila wilaya- Serikali

MAHAKAMA ya Tanzania imeandaa Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) ambao utahakikisha mikoa, wilaya na makao makuu ya tarafa yanakuwa na mahakama nchini.

Kauli hiyo ametoa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geoffrey Pinda wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Kalambo, Josephat Kandege (CCM) aliyehoji ni lini itapeleka mahakimu katika tarafa zenye majengo ya mahakama na pia lini itajenga mahakama ya wilaya ya Kalambo.

Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Pinda amejibu kwamba wizara yake itahakikisha inatuma mahakimu katika mahakama za tarafa zenye majengo na pia itajenga mahakama za wilaya ya Kalambo kama mpango unavyoonesha.

Pia Pinda ametoa jibu hilo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Easter Bulaya (Chadema) aliyetaka kujua ni lini serikali itajenga mahakama ya wilaya ya Bunda na kuachana kupanga jengo la mzee Steven Wassira na mahali pengine?

Pinda amesema ni kweli mahakama nyingi nchini zimekuwa zikipanga, lakini ni mkakati wa wizara kuhakikisha ifikapo mwaka 2025/26, kero ya kupanga inakwisha wanakuwa na majengo yao.