Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 28Article 540367

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: ippmedia.com

Ijue siri mishahara watumishi wa umma kutopandishwa miaka sita

Kila upande unaohusiana na hoja hiyo, kuanzia wanaoguswa moja kwa moja na walio nayo kwa jirani, unawasilisha utetezi uliobeba mashiko kwa namna yake.

Ni kwa namna gani? Wakati mwajiriwa wa serikalini analia kutopatiwa haki yake ya kupandishwa cheo kwa muda mrefu, mwajiri anakiri ukweli huo, lakini kwa upande wa pili wa shilingi anasimama katika tafsiri 'haiwezekani kwa sasa kutokana na ugumu wa uchumi'.

Je, kupanda cheo kuna maana gani? Sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2003 inatoa tafsiri kwamba: "Kupanda cheo ni kutoka ngazi moja kwenda kwenye ngazi ya juu yake kikazi".

Tafsiri hiyo yenye ufafanuzi katika Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009, inadokeza kuwa ni mabadiliko yanayoendana na ongezeko la mshahara kwa mnufaika.

Miongozo hiyo ya kisheria inaorodhesha vigezo muhimu vya kufikia uamuzi wa upandishaji vyeo na yanayoambatana nayo, ikijumuisha kuwapo nafasi zilizo wazi na zimeidhinishwa kisheria au kiutaratibu.

Vingine ni bajeti kuruhusu uwezekano huo, mlengwa kuwa na sifa ya utendaji kazi unaokidhi mahitaji kwa mujibu wa Tathmini ya Wazi ya Utendaji Kazi (OPRAS) na sifa hitajika kwa nafasi anayoelekezwa.

MVUTANO ULIPO

Wakati pande zote (mwajiri na mwajiriwa) wanakubaliana na vigezo vilivyopo, bado utekelezaji wake umebaki mgumu, kila mmoja ana utetezi wake anaouamini uko sahihi.

Hadi sasa ni hoja inayochukua sura pana, huku ulingo wa siasa uliobaki kando kwa muda, nao ukiingia, ikiwamo bungeni.

Watumishi wa umma kupitia mwakilishi wao, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Kitaifa mwezi huu jijini Mwanza, Kaimu Katibu Mkuu, Said Wamba, alilalamika kutimu miaka sita pasipo kada hiyo kupandishwa vyeo na mishahara.

Ndani ya hafla hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan, akawarejeshea ufafanuzi akikubaliana nao, lakini akiwaanikia uhalisia uliopo kwamba haiwezekani kwa sasa na akawaahidi kuliangalia hadi maadhimisho yajayo.

Hoja hiyo ya Mkuu wa Nchi inatetewa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, akiwa na ufafanuzi kuwa sehemu kubwa ya bajeti ya nchi inaelekezwa kugharamia madeni na mishahara ya watumishi wa umma.

Dk. Mpango ambaye ni mwanazuoni mchumi kitaalamu, aliyetumikia mashirika ya fedha kimataifa na pia kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, anasema makusanyo ya nchi ni wastani wa Sh. trilioni 1.3 kwa mwezi na matumizi, wastani Sh. bilioni 600 hulipa madeni ya serikali huku mishahara ikichukua Sh. bilioni 550 katika muda huo.

Kiasi kidogo kinachobaki (takribani Sh. bilioni 150) kinatumika kugharamia huduma kama vile elimu, matibabu ya wazee na upanuzi wa miradi ya afya.

Muda mfupi baada ya kuapishwa kuwa Makamu wa Rais, Dk. Mpango aliitaka Mamlaka ya Mapato (TRA) kuongeza jitihada katika ukusanyaji wa mapato ili wafike wastani wa Sh. trilioni mbili kwa mwezi.

ANGALIZO LA CAG

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, anatahadharisha kuwa hali hiyo ikiendelea, kutakuwa na utendaji duni miongoni mwa watumishi.

Katika ripoti yake ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2019/20 iliyowasilishwa bungeni mwezi uliopita, CAG Kichere anabainisha kuwa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 zinataka tarehe ya kupandishwa daraja ya mtumishi wa umma iamuliwe na mamlaka sahihi.

"Kinyume cha kanuni hizo, nilipitia mafaili ya watumishi pamoja na mfumo wa LAWSON wenye taarifa mbalimbali za watumishi na kubaini kuwa watumishi 7,992 katika mamlaka 14 za serikali za mitaa hawakupandishwa madaraja ingawa walikuwa na sifa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma.

"Kushindwa kupandisha madaraja na kutoa nyongeza ya mishahara kwa wakati kwa watumishi wa umma husababisha utendaji duni katika utoaji wa huduma na hii huhatarisha nia njema ya serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi," CAG anatahadharisha.

HOJA BUNGENI

Nje ya ulingo wa wanaodai, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), anabeba bango la kilio cha wafanyakazi, akiwatetea kwamba ni muda mrefu wamesahaulika stahiki zao.

Pendekezo lake bungeni kuwatetea watumishi wa umma ni kuitaka serikali kuunda tume kuchunguza undani wa kusahaulika huko, kupunjwa mafao na stahiki zingine rasmi.

Ni hoja inayopatiwa sehemu ya ufafanuzi nje ya Bunge, Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Jayne Nyimbo-Taylor, akidokeza undani wa magumu yanayowakabili, akitaja mzigo wa mlundikano wa kodi.

Mwakilishi huyo wa kada ya waajiri nje ya serikali, anapendekeza haja ya kuwapo umakini katika marekebisho ya sheria ili yasiathiri uendeshaji taasisi kwa waajiri.

Vilevile, waziri mwenye dhamana na utumishi wa umma, Mohamed Mchengerwa, katika majibu yake bungeni ndani ya kipindi mfupi tangu kuteuliwa kushika nafasi hiyo, anatoa faraja kufanyia kazi hoja zenye sura ya kilio cha utumishi kwamba kutafanyika mapitio ili kutoa haki kwa wanaostahili.

''Kwa miaka sita watumishi wa umma hawajaongezwa mishahara yao na wale wa sekta binafsi mishahara yao haijaongezwa kwa miaka minane sasa," Rais Samia alisema.

*ITAENDELEA KESHO

Join our Newsletter