Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 28Article 540271

xxxxxxxxxxx of Friday, 28 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Jafo azitaka asasi kulinda mazingira

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo amezitaka asasi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na hifadhi na usimamizi wa mazingira zishiriki kusimamia na kulinda mazingira nchini.

Jafo alisema hayo jana jijini Dodoma katika kikao maalumu cha kujadili mchango na majukumu ya asasi hizo katika hifadhi na usimamizi wa mazingira.

Alisema lengo la serikali ni kuhamasisha utendaji kazi wa asasi hizo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na kudumisha uhusiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na asasi hizo.

“Leo ni siku ya ndoto yangu kukutana na wadau muhimu katika kusukuma mbele ajenda ya mazingira, hii inanipa faraja kubwa kuona tunao wadau wengi sana wenye nia ya dhati katika kusukuma mbele ajenda hii muhimu,” alisema.

Jafo alisema bajeti ya mazingira ni ndogo na kutoa rai kwa wadau wazingatie zaidi usimamizi wa mazingira kwa kushirikiana na serikali ili kuratibu shughuli za mazingira kwa ufanisi.

“Nafahamu mmekuwa wadau wakubwa katika hifadhi ya mazingira nchini na mmekuwa mkijitoa katika maeneo mbalimbali pamoja na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu ajenda hii muhimu ya mazingira kwa mustakabali wa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Jafo.

Alizitaka asasi hizo zisogeze huduma katika maeneo mengi nchini ili kuwe na tija katika kupambana na uharibifu wa mazingira.

“Hatuwezi kupata uchumi endelevu bila kudhibiti mazingira yetu, uharibifu wa mazingira duniani ni wa kutisha, athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa na kumekuwa na ongezeko la kina cha maji katika mito, mabwawa na maziwa kutokana kuongezeka kwa mvua juu ya wastani,” alisema.

Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga alisema serikali na asasi za kiraia zinapaswa kufanya kazi pamoja kwa kuzingatia misingi ya uwazi, uadilifu, sera, sheria, taratibu na miongozo ya serikali katika kulinda mazingira.

Join our Newsletter