Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 06Article 561616

Habari Kuu of Wednesday, 6 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Jaji Mkuu: "Tanzania hakuna sheria mbaya"

JAJI Mkuu, Profesa Ibrahim Juma JAJI Mkuu, Profesa Ibrahim Juma

JAJI Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, amesema sheria zilizopo nchini si mbaya hivyo wananchi wazisome waelewe kabla ya kutaka zibadilishwe.

Profesa Juma alisema hayo wakati wa hafla ya kumuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi kuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

"Ningependa kuwaambia Watanzania wenzangu, Sheria za Tanzania si mbaya, nafsi ndiyo mbaya. Sheria hii hii ukiipeleka Marekani itafanya kazi vizuri sana,” alisema na kuongeza:

"Pengine badala ya kufikiria kufanya mabadiliko ya sheria, tuanze kufikiria mabadiliko ya nafsi. Nafsi zetu zinaheshimu sheria? Nafsi zetu zinafuata utaratibu? Kwa sababu bila sisi wenyewe kufuata utaratibu, hata tukiwa na sheria nzuri namna gani haitasaidia," alisema.

Profesa Juma alisema kabla ya wananchi kuhitaji mabadiliko ya sheria au Katiba wasome kwanza vifungu husika ili kuelewa kama kuna changamoto.

Alisema hakuna aliye juu ya sheria na kuna utaratibu wa kushughulikia hata nidhamu kwa mahakimu na majaji na kuna mifumo ya kuwasilisha malalamiko.

"Ukiangalia sheria inayoendesha shughuli za mahakama imeunda kamati za maadili. Kuna Kamati za Maadili za Majaji, ambazo zinapokea malalamiko ya kinidhamu dhidi ya Majaji wa Rufani, Jaji Kiongozi na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wake ni Jaji wa Mahakama ya Rufani," alisema.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Feleshi, alisema uapisho huo unamkumbusha namna alivyokuwa akitekeleza majukumu yake katika ngazi mbalimbali kabla na baada ya kuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

"Nashukuru kwa dhamana nyingine ya kuwa mjumbe wa tume hii nikiwa kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hii ni heshima kubwa kwangu kwa kuaminiwa," alisema.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, alimpongeza Feleshi kwa kuapishwa kuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.