Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 20Article 573070

Habari za Mikoani of Saturday, 20 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kahama yapata bil 34.8/za dhahabu robo mwaka

Kahama yapata bil 34.8/za dhahabu robo mwaka Kahama yapata bil 34.8/za dhahabu robo mwaka

OFISA Madini Mkoa wa kimadini Kahama, Jeremiah Hango amesema kuwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2021/2022 wamefanikiwa kukusanya Sh bilioni 34.8 sawa na asilimia 110 na kuvuka lengo walilokuwa wamepangiwa na serikali la kukusanya Sh bilioni 31.7 kutokana na madini.

Alisema hayo jana alipokuwa akitoa taarifa fupi kwenye kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya katika soko la madini ya dhahabu huku akieleza kuwa kuna jumla ya madalali 60 na wanunuzi 38.

Hango alisema kuwa soko la madini lilianzishwa mwezi Julai mwaka 2016 kwa sheria ya mwaka 2010 na marekebisho yake kufanyika mwaka 2017 huku kukiwa na masoko madogo madogo maeneo sita yaliyotengwa kwa mujibu wa sheria.

“Ukusanyaji wa mapato yameongezeka kwenye robo hii ya kwanza kwa kilo 60.78 ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka jana kuanzia mwezi Julai hadi Oktoba na wanaokwenda kutafuta wateja kwenye uchimbaji ni kukiuka sheria na kuwa inatakiwa wafuate masoko yalipo,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga alisema utafiti unaonesha dhahabu haijapungua ndio maana mapato yameongezeka na kunatakiwa wanunuzi, madalali na wachimbaji wawe na weledi mkubwa na wasivunje sheria zilizowekwa.

“Tukienda vizuri katika ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha mwaka mzima tunaweza kufikia Sh bilioni 200, serikali inawaheshimu wachimbaji wadogo na wanunuzi, kwa sababu mchango wenu ni mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi kwa kulipa mapato serikalini,” alisema.

Mwenyekiti wa wanunuzi wa madini ya dhahabu mkoani hapo, Emanuel Kidenya aliomba kamati ya ulinzi na usalama kuwahakikishia usalama wao wanaposafirisha madini kwenda sokoni. Alionya madalali wanaokwenda kuvizia wateja kwenye uchimbaji kwa kuwataka waache mara moja.

Mnunuzi wa dhahabu, Abdulhaman Sangey aliiomba serikali kuwaweka pamoja na taasisi za kifedha karibu na maeneo ya ununuzi wa dhahabu kwa usalama wao.