Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 19Article 572758

Habari Kuu of Friday, 19 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Kampuni 174 mpya za Tanzania zameajiri watu 57,650

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, amesema kampuni 174 zimesajiliwa katika maeneo ya EPZ na SEZ na kuwekeza mtaji wa Dola za Kimarekani bilioni 2.23.

Amesema kupitia uwekezaji huo jumla ya ajira 57,563 zimezalishwa, hivyo kuwanufaisha Watanzania wengi.

Prof. Mkumbo alibainisha hayo juzi jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya sekta za viwanda na biashara katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika.

Alisema serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji kwenye maeneo ya EPZ/SEZ ili kuhakikisha mazao ya kilimo, misitu, mifugo, uvuvi na madini yanayozalishwa nchini yanaongezwa thamani na kutengeneza ajira kwa Watanzania badala ya kusafirishwa kama malighafi kwenda nje.

“Kwa sasa serikali inaendelea na majadiliano na mwekezaji ambaye ni kampuni ya CMPort kutoka China na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman ili ujenzi wa eneo maalum la kiuchumi Bagamoyo (Bagamoyo SEZ) uanze mapema iwezekanavyo,” alisema.

Pia alisema mchango wa sekta ya viwanda kwenye pato la taifa umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo wakati wa uhuru mwaka 1961 sekta ya viwanda ilikuwa ikichangia asilimia 3.5 ya pato la taifa.

“Hadi kufikia mwaka 2015 mchango wa sekta hiyo ulikuwa asilimia 7.9 kutokana na jitihada ya serikali za kuhamasisha ujenzi wa viwanda mchango wa sekta ya viwanda kwenye pato la taifa uliongezeka na kufikia asilimia 8.5 ya pato la taifa. Mwaka 2019 na mwaka 2020 mchango wa sekta ulishuka kidogo hadi asilimia 8.4”alisema.

Kuhusu mchango wa sekta ya viwanda kwenye ajira alisema imeendelea kuongezeka ambapo mwaka 1961, ilichangia asilimi tisa ya ajira zote nchini.

“Hadi kufikia mwaka 2015, ajira katika sekta ya viwanda zilikuwa zimeongezeka na kufikia 254,786. Aidha kutokana na msukumo mkubwa wa ujenzi wa uchumi wa viwanda, idadi ya ajira imeongezeka zaidi na kufikia ajira 482,601 mwaka 2021,” alisema Prof. Mkumbo.

Pia alisema wizara hiyo imeandaa mwongozo wa uwekezaji katika mitaa ya viwanda nchini ili kurahisisha taratibu za uwekezaji katika mitaa ya viwanda na kuongeza kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.