Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 04Article 540931

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kampuni Korea Kusini yazipa umemejua shule

KAMPUNI ya Yolk ya nchini Korea Kusini imesambaza umeme wa jua ujulikanao kwa jina la ‘Solar Cow’ katika shule nane za msingi wilayani Monduli.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yolk, Jeon Only, alisema lengo la kampuni hiyo kuweka umeme utokanao na mionzi ya jua katika shule hizo ni kuhamahisha watoto wa jamii ya wafugaji wa Kabila la Wamaasai kupenda shule na kuacha kuchunga mifugo na kuolewa kabla ya muda.

Alisema baada ya kuweka umeme huo katika shule hizo, wataangalia uwezekano na kuanza mchakato wa kuweka umeme huo katika shule zote za msingi wilayani Monduli.

Only alisema hayo katika Shule ya Msingi Lengijabe iliyopo Kata ya Lemoot wilayani Monduli, baada ya kukabidhi vifaa na mitambo ya umeme zaidi ya 300 katika shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 535.

Alisema wanafunzi wengi wa jamii ya kifugaji ni watoro na kwamba, baadhi ya wazazi wanachangia utoro huo kwa kuwapa kazi za kuchunga mifugo huku wakiwazuia watoto wa kike kwenda shule ili waolewe ingawa ni wadoga.

Kwa mujibu wa Only, watasambaza mitambo ya kuzalisha umeme jua katika shule za msingi wilayani Monduli na baadaye, watafanya hivyo katika wilaya nyingine za Mkoa wa Arusha kama watapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa hatua ya pili ya kusaidia elimu katika Wilaya ya Monduli ni kujenga shule ya sekondari na ufundi katika Kata ya Loksale ili kuinua elimu kwa jamii hiyo.

Akipokea vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Stephen Ulaya, alisema jitihada zinazofanywa na Kampuni ya Yolk zinapaswa kupongezwa kwani ni uamuzi mzuri unaolenga kuendeeza elimu kwa jamii ya wafugaji ya Kimaasai.

Ulaya alisema tatizo kubwa kwa jamii hiyo ya wafugaji wa Kimaasai ni utoro kwa watoto kutokana na kuoewa kazi za kuchunga huku watoto wa kike wakipaswa kuolewa jambo analosema kuanizhswa kwa mradi huio kutachangia kukomesha hali hiyo.

Ofisa Elimu (Msingi) wa Wilaya ya Monduli, Richard Kipepeto, alisema hatua ya kila shule kuwekwa umeme jua inaweza kuongeza ufaulu kwa jamii ya kifugaji na kufanya jamii hiyo kuondoana na utegemezi.

Join our Newsletter