Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 10Article 546301

Habari Kuu of Saturday, 10 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Katibu Mkuu UN ampongeza Samia

Katibu Mkuu UN ampongeza Samia Katibu Mkuu UN ampongeza Samia

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri tangu ashike nafasi ya urais.

Salamu za mtendaji huyo wa UN ziliwasilishwa jana na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Joyce Msuya aliyefanya mazungumzo na Rais Samia Ikulu, Dodoma jana.

“Naibu Mkurugenzi huyo wa UNEP ametoa salamu za pongezi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa…na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Amina Muhammed kwa Rais Samia kwa uongozi wake mahiri tangu ashike nafasi ya urais nchini Tanzania,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Msuya alisema UNEP Kwa kushirikiana na UN wako tayari kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika maendeleo na mipango yake ya kutunza na kuhifadhi mazingira.

Pia alimpongeza Samia kwa jitihada anazochukua kukabiliana na ugonjwa wa covid-19 na kusema Umoja wa Mataifa uko tayari kuunga mkono jitihada hizo.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Christine Musisi alisema kupitia mpango mkakati wa miaka mitano wanaouandaa, utazingatia mpango wa maendeleo wa tatu wa miaka mitano (FYDP III) wa Tanzania.

Rais Samia alishukuru na kuahidi kuendelea kushirikiana na UNEP katika mipango thabiti ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira nchini.

Alitaka UN kuhakikisha kuwa mpango wao wa miaka mitano wanaouandaa unakuwa endelevu na wenye kuleta tija katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Samia alisema serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kukabiliana na uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira bora wananchi katika kushughuli zao za maendeleo ili wasizidi kuharibu mazingira.

Aliwaomba UNEP kwa kushirikiana na UN kuendeleza jitihada za Serikali kwa kuwapatia rasilimali fedha na raslimali watu ili azma ya kutunza mazingira ifanikiwe kikamilifu.