Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 19Article 572695

Habari Kuu of Friday, 19 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Kauli ya Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kuhusu Mahakama za Tanzania

Kauli ya Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kuhusu Mahakama za Tanzania Kauli ya Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kuhusu Mahakama za Tanzania

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia maendeleo ya kisera na ushirikiano, Mari Pangestu ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuboresha huduma kwa wananchi. Pangestu alitoa pongezi hizo baada ya kukutana na kuzungumza na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na kutembelea kituo jumuishi cha masuala ya familia kilichopo Temeke, Dar es Salaam.

Pia alipata maelezo ya huduma za mahakama inayotembea na akapokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maboresho wa huduma za mahakama wa mwaka 2015/2016- 2019/2020 iliyowasilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Zahra Maruma.

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter, Pangestu alieleza kufurahishwa na huduma za mahakama inayotembea. “Nilifurahi sana kuona jinsi Mahakama ya Tanzania inavyotoa huduma zake kwa wananchi wakiwemo wanawake na watoto kupitia mahakama inayotembea ambayo ilipatikana kwa msaada wa fedha kutoka Benki ya Dunia,” alisema.

Mahakama hiyo ilianza kutoa huduma Julai, 2019 na hadi sasa imesikiliza na kumaliza zaidi ya mashauri 1,600. Mahakama hiyo pia inatoa elimu ya sheria/ ushauri bure wa kisheria katika maeneo ambayo yapo mbali na mahakama. Pangestu pia alipongeza utoaji wa huduma kwenye vituo jumuishi vya utoaji haki vilivyozinduliwa Oktoba 6 mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Tumetembelea kituo jumuishi cha masuala ya familia-Temeke, moja ya vituo sita vilivyojengwa na Benki ya Dunia, kituo hiki kinatoa huduma mbalimbali za haki chini ya paa moja, huduma hizo ni pamoja na masuala ya talaka, mirathi,” alisema. Pangestu aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuboresha huduma kupitia mradi wa uboreshaji huduma za mahakama uliofadhiliwa na fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Hivi sasa mahakama inaendelea na awamu ya pili ya utekelezaji wa mpango mkakati wa pili wa uboreshaji wa huduma za mahakama wa mwaka 2020/2021-2024/2025.