Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 22Article 559015

Dini of Wednesday, 22 September 2021

Chanzo: globalpublishers.co.tz

Kauli ya Sheikh Mkuu wa DSM kuhusu watu kujiita Maaskofu bila taratibu

SHEIKH wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Alhad Mussa Salum SHEIKH wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Alhad Mussa Salum

SHEIKH wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Alhad Mussa Salum amebainisha mambo mawili ambayo dini za Kiislamu na Kikristu zinatofautiana huku akisema “kuupata uaskofu wa Kanisa Katoliki ni gharama na kazi kubwa.” 

Amesema hayo jana Jumanne, tarehe 21 Septemba 2021, katika misa takatifu ya kuwekwa wakfu kwa mapadre wawili Stephano Msomba na Henry Mchamungu kuwa Maaskofu wasaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Maaskofu hao wapya, wamewekwa wakfu na Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Jude Thadeus Ruwa’ichi katika viwanja wa Msimbazi Center.

Misa hiyo imehudhuriwa na maaskofu, mapadre, watawa na viongozi mbalimbali wa kiserikali, siasa, waumini na viongozi wa dini.

Sheikh Alhad alikuwa miongoni mwa waliohudhuria misa hiyo na kupewa fursa ya kuzungumza na hadhira iliyokuwepo akiwa na dhamana pia kama mwenyekiti wa kamati ya amani ya mkoa huo.

Ameanza kwa kushukuru kupewa fursa ya kuzungumza, jambo hili ni kubwa na heshima kubwa kama mwenyekiti wa kamati ya amani na jumuiya ile ya maridhiano kuwepo hapa kushuhudia misa hii ya wasaidizi wa Askofu Ruwa’ichi wakisimikwa.

Sheikh Alhad amesema, mara baada ya kupata mwaliko wa kuhudhuria shughuli hii, aliwasiliana na Mufti Abubakar Zubeir ambaye alimruhusu kufika pasina kukosa huku akisema “nikirudi nitamfikishia salamu.”

Akiendelea kuzungumza amesema, “Kanisa Katoliki ndilo kanisa halisi linaloonesha ukiristo wa kwelikweli. Nimejifunza nidhamu ya hali ya juu ya mababa askofu, nidhamu ya hali ya juu kwa waumini dhidi ya viongozi wake.”

Sheikh Alhad ametumia fursa hiyo kukumbushia mkutano wa viongozi wa dini uliofanyika wakati wa utawala wa awamu ya nne na kufunguliwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete katika Hotel ya White Sands.

Amesema, katika mkutano huo, Wakristu walitakiwa waeleze mambo mawili wanayopenda kutoka kwa Waislamu na Waislamu waeleze mambo mawili wanayopenda kutoka kwa Wakristu.

Huku vicheko vikisikika na wengine wakishangilia, Sheikh Alhad amesema, wenzetu Wakristu walisema “tunapenda sana pale wanapotekeleza ibada zao za swala tano kwa wakati ni jambo jema sana kwa Waislamu.”

Yuda Thadei Rwaichi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam

“Lakini unapoingia mwezi mtukufu wa Ramadhan, wanakuwa wema zaidi, wakarimu, watulivu na hata baa wanapungua mtaani,” amesema Sheikh Alhad na kuibua shangwe kutoka kwa wahudhuriaji wa misa hiyo.

Kisha akaendelea kubainisha mambo mawili ya Wakristu akisema “sisi Waislamu tukataja na mambo mawili, tukasema katika huduma za jamii wametushinda, wako vizuri sana katika elimu, afya na sisi mashekh tunakiri hili.”

Jambo la pili, “tunaheshima, nidhamu ya waumini kwa viongozi wao.”

Akiendelea kuzungumza, Sheikh Alhad amesema kuupata uaskofu ndani ya Kanisa Katoliki si jambo jepesi.

“Hata mababa maaskofu walivyovaa, namna walivyopendeza. Nilikuwa nadhani ni rahisi tu unakwenda Kariakoo ukanunua tu, kumbe ni kitu kinapatikana kwa kazi kweli kweli siyo kitu rahisi. Unaanza utaratibu wa ndani.

“Tuna shida kubwa na msiba mkubwa, mitaani mtu anajipa tu uaskofu na kutishatisha watu, kumbe hata uchungaji hajapitia, baba askofu nimejifunza uaskofu ni kazi kubwa,” amesema Sheikh Alhad.