Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 20Article 558658

Uhalifu & Adhabu of Monday, 20 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Kesi ya Mbowe: Maswali ya Wakili Kibatala kwa Inspekta Mahita

Freeman Mbowe na Wakili Peter Kibatala. Freeman Mbowe na Wakili Peter Kibatala.

WAKILI anayeongoza jopo la mawakili wa utetezi katika shauri dogo la kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, Peter Kibatala amehoji kama polisi aliyehusika katika ukamataji wa washtakiwa wawili katika kesi hiyo, anatoka Kikosi cha Polisi cha Kuzuia Ugaidi.

Wakili Kibatala amehoji hayo leo Jumatatu, Septemba 20, 2021, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Mustapha Siyani.

Washtakiwa hao wawili waliokamatwa maeneo ya Rao mkoani Kilimanjaro Agosti 2020, kwa tuhuma za kujihusisha na kosa la kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi ni Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Akimhoji shahidi wa pili wa Jamhuri katika shauri hilo dogo, Inspekta Mahita Omari Mahita, aliyekuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Wakili Kibatala alimuuliza kama kuna kikosi maalum kinachoshughulika na makosa ya ugaidi, ambaye alijibu hafahamu.

Wakili Kibatala alimhoji Inspekta Mahita, kama na yeye ni miongoni mwa wahusika wa kikosi hicho, ambaye alijibu hapana. Wakili Kibatala alimhoji swali hilo Inspekta Mahita, kwa kuwa alikuwa miongoni mwa Askari Polisi waliyoshiriki zoezi la kuwakamata watuhumiwa hao.

Mbali na kuhoji hayo, Wakili Kibatala alimtaka Inspekta Mahita, aieleze mahakama hiyo kama inaruhusiwa kutumia bisibisi kumtisha mtuhumiwa aliyekamatwa, ambaye alijibu akidai hairuhusiwi.

Pia, Kibatala alimhoji Inspekta Mahita akidai kama inaruhusiwa mtuhumiwa kufungwa pingu mikononi na miguuni sambamba na kupewa mateso hadi kushindwa kitembea, ambapo alijibu akidai hairuhusiwi.

Wakili Kibatala alimhoji Inspekta Mahita akidai kama anafahamu mtuhumiwa wa pili, alifungwa machoni kwa kutumia jaketi lake jekundu, ambaye pia alijibu akidai hafahamu.

Shauri hilo lilitoka na mapinganizi ya Mawakili wa utetezi, wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, wakipinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi ya msingi, Adam Kasekwa, yasitumike mahakamani hapo kama kielelezo na Kamanda Kingai, katika kesi ya msingi, wakidai yalichukuliwa nje ya muda kisheria.

Pia, katika mapingamizi hayo walihoji kwa nini mtuhumiwa alihojiwa Dar es Salaam, badala ya Moshi mkoani Kilimanjaro alikokamatwa.