Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 10Article 556594

Habari Kuu of Friday, 10 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kesi ya Mbowe na wenzake kuendelea leo Mahakama Kuu

Kesi ya Mbowe na wenzake kuendelea leo Mahakama Kuu Kesi ya Mbowe na wenzake kuendelea leo Mahakama Kuu

KESI ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu itaanza kusikilizwa leo mbele ya Jaji Mustapha Siyani.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Magdalena Ntandu alisema jana kuwa kesi hiyo itasikilizwa katika muda wa kazi.

Kesi hiyo ilipaswa kuanza kwa kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali baada ya kusomewa maelezo ya mashahidi lakini upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala ulipinga hatua hiyo.

Upande huo uliwasilisha mapingamizi yenye hoja nne kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba hati ya mashitaka ni batili na ukaomba mashitaka yafutwe.

Hata hivyo, upande wa mashitaka ulipinga hoja hizo ukidai mahakama hiyo ina mamlaka na hati ya mashitaka iko sahihi.

Kutokana na hali hiyo Jaji Elinazer Luvanda alitupilia mbali mapingamizi yote hata hivyo, haikuendelea baada ya Mbowe kudai hawana imani na jaji huyo katika kutenda haki.

Jaji Luvanda alikubaliana na ombi la mshitakiwa huyo wa nne la kujitoa kusikiliza kesi hiyo. Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Hassan, Adamu Kasekwa, na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.