Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 30Article 554389

Habari Kuu of Monday, 30 August 2021

Chanzo: ippmedia.com

Kesi ya uhujumu uchumi na ugaidi dhidi ya Mbowe kutikisa kesho

Mbowe Mbowe

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kesho inatarajia kuanza kusikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Kesi hiyo ambayo washtakiwa walisomewa maelezo ya mashahidi Agosti 23, mwaka huu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Elinaza Luvanda.

Upande wa Jamhuri unatarajia kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali dhidi ya mashtaka sita ya ugaidi yanayowakabili.

Katika shauri hilo la uhujumu uchumi namba 16/2021 upande wa mashtaka unatarajia kuita mashahidi 24 akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz.

Jamhuri inawakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, Jenitreza Kitali na Esther Martin.

Mbowe na wenzake watatu wanawakilishwa na Wakili Peter Kibatala, John Mallya, Jebra Kambole, Frederick Kihwelo, Lwekamwa Rweikiza na Marie Mushi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbowe, Halfan Bwire, Adam Kasekwa, maarufu Adamu na Mohamed Ling'wenya, ambao wanakabiliwa na mashtaka sita.

Katika shtaka la kwanza wanadaiwa wote, walikula njama kati ya Mei Mosi na Agosti Mosi 2020 katila Hoteli ya Aishi iliyopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro na maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, kulipua vituo vya mafuta kuhatarisha usalama wa Taifa na kusababisha hofu kwa jamii.

Shtaka la pili wote wanadaiwa kula njama kufanya vitendo vya kigaidi na kutaka kumsababishia majeraha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Sabaya.

Shtaka la tatu, Mbowe anadaiwa katika kipindi hicho na mahali hapo aliwawezesha kifedha Halfani, Adamu na Ling'wenya huku akiamini fedha hizo zitasaidia katika kufanya ugaidi

kwa kulipua vituo mbalimbali vya mafuta na mikusanyiko kwa lengo la kuharibu misingi ya kisiasa, katiba, uchumi na sifa ya Jamuhuri ya Mauungano wa Tanzania.

Shtaka la nne wanadaiwa kushiriki vikao vya kufanya vitendo vya kigaidi.

Shtaka la tano, mshtakiwa Adamu anadaiwa Agosti 5, mwaka 2020 eneo la Rau alikutwa na bastola yenye namba A 5340 aina ya Luger.

Mshtakiwa Halfani katika shtaka la sita anadaiwa Agosti 10, mwaka 2020, kwa lengo la kuhatarisha usalama wa nchi alitumia sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) ambazo ni suruali moja ya JKT, pamoja na suruali nne za JWTZ, fulana moja, koti la mvua moja, jacket moja, kofia tano, overall tano, begi la kubebea vifaa vya JWTZ lijulikanalo kwa jina la ponjoo, vyeo vinne vya koplo, mikanda minne, soksi jozi moja,sweta, begi la mafunzo ya parachuti, kibuyu cha kunywea maji pamoja na kisu aina ya AK 47 CCCP, vyote vya JWTZ.

Shahidi wa kwanza anatarajia kuwa

Kamishna wa Polisi Robert Boaz ambaye katika ushahidi wake uliosomwa Mahakama ya Kisutu anadai Julai mwaka 2020 alipokea simu kutoka kwa mtu asiyemfahamu akamwambia kuna uhalifu umepangwa kufanyika kwa ajili ya kudhuru viongozi wa serikali.

Anadai mtu huyo alijitambulisha kuwa ni Luteni Denis Urio, alimwambia aende ofisini kwake, alienda akampa taarifa kuwa Mbowe anataka amtafutie wanajeshi wastaafu, makomandoo au waliofukuzwa kazi ili ashirikiane nao kuwazuru viongozi akiwamo Sabaya.

Boaz anadai alimwambia Luteni usijitoe aendelee kumtafutia watu, alimtafutia watu wawili, mpango wa kumdhuru Sabaya ulikamilika, watuhumiwa walikamatwa mkoani Kilimanjaro, alifanya upelelezi kubaini uhusika wa Mbowe wakabaini kwamba yeye ndiye kinara.

Luteni Urio katika ushahidi wake anadai anaishi Morogoro Kihonda, Ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania kikosi 92 KJ, mstaafu na alimfahamu Mbowe, walikutana Mikocheni mwaka 2012, alimweleza harakati za ukombozi wa nchi.

Siku nyingine Mbowe alimpigia simu alitaka wakutane akasema hana nafasi, Mbowe alikataa kuzungumza kwa simu kutokana na aina ya mazungumzo.

Julai mwaka 2020 walikutana maeneo ya Mikocheni, Mbowe akamwambia kwamba CHADEMA kitachukua dola, Luteni Urio atapewa nafasi ya juu hivyo amtafutie mwanajeshi waliofukuzwa kazi, makomandoo na wastaafu ili wamsaidie katika harakati za kuchukua Dola.

"Niliamua kumpigia DCI Boaz nilimsimulia kwa sababu mimi ni mlinzi wa nchi yangu, Boaz akaniambia kila hatua watakayokuwa wanaifanya kina Mbowe niwe natoa taarifa.

"Mbowe alinitumia Sh. 500,000 kwa simu yake nikatoa Sh. 300,000 nikampa Halfani Bwire ikabaki katika simu Sh. 195,000, akatuma tena Sh. 199,000.

"Baada ya hapo Mbowe akakata mawasiliano na mimi, nikaamua kuwasiliana na Bwire kujua kinachoendelea," anadai katika ushahidi wake.

Anadai Bwire alimfahamisha kuwa wanatakiwa kumdhuru Sabaya kabla ya Agosti 7, 2020, walikuwa wanatumia mawasiliano ya telegrams kwa madai ndio salama.

Baadhi ya mashahidi wengine ni ASP Ramadhani Kingai, Mrakibu wa Polisi (SP) Jumanne, Inspekta Omari Mahita, Justine Kahaya alikuwa msaidizi wa Sabaya kabla ya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai.

Upande wa utetezi unadai miongoni mwa mashahidi wao ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya.