Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 03Article 567865

Habari Kuu of Wednesday, 3 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

Kilichosababisha msanii Vitali kukamatwa hiki hapa

Msanii, Vitali Maembe Msanii, Vitali Maembe

Siku moja baada ya msanii Vitali Maembe kukamatwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Bagamoyo, Chama Cha ACT-Wazalendo kimedai kuwa msanii huyo alikamatwa kwa tuhuma za kuwakashifu viongozi kupitia wimbo wake wa Kaizari.

Hayo yamelezwa leo Jumatano Novemba 3, 2021 katika taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu na Makundi Maalumu Taifa Chama cha ACT- Wazalendo, Mbarala Maharagande.

Taarifa hiyo imesema kuwa, Maembe ambaye pia ni mwanachama wa chama hicho alikamatwa jana Bagamoyo na baadaye kuhamishiwa Kibaaha.

“Maembe ambaye jana tarehe 02, Novemba 2021 alishikiliwa na Jeshi la Polisi Bagamoyo kisha baadaye kuhamishiwa Kibaha, amehojiwa na Jeshi hilo kwa tuhuma ya kuwakashifu viongozi kupitia nyimbo yake ya Kaizari” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mwanasheria wa chama hicho, Bonifasia Mapunda amefika Kibaha na kuzungumza na Maembe pamoja na uongozi Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa lengo la kufuatilia na kuhakikisha kuwa msanii huyo anaachiwa huru.

Wakati ACT-Wazalendo wakitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa waPwani, Wanko Nyigesa amesema bado wanafuatilia taarifa za kukamatwa kwa msanii huyo.

Mwaka 2020 mkali huyo wa kibao cha 'Sumu ya Teja' aligombea ubunge katika Jimbo la Bagamoyo kwa tiketi ya ACT-Wazalendo.