Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 30Article 540634

xxxxxxxxxxx of Sunday, 30 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kilimo kusaidia wakulima wa pareto kufikisha tani 9,000

TANZANIA imedhamiria kuendelea kuongoza barani Afrika kwa uzalishaji wa zao la pareto kutoka tani 3,000 mwaka 2021 hadi kufikia malengo ya tani 9,000.

Hayo yalibainishwa juzi jijini Dodoma wakati wa kikao cha wadau wa zao la pareto kutoka mikoa sita nchini kilichoshirikisha viongozi wa mikoa, wilaya ,halmashauri, kampuni za pareto na wawakilishi wa wakulima.

Akizungumza kwenye kikao hicho Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliwapongeza wadau kwa kuweka lengo hilo la kufikisha tani 9,000 za maua ya pareto ambapo viwanda vitatu vilivyopo sasa vitaweza kuinunua yote kulingana na uwezo wake.

Bashe alisema ili kufikia malengo hayo ya uzalishaji wizara kupitia Bodi ya Pareto na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) itawekeza kwenye utafiti wa mbegu bora za pareto na kuhakiki-

sha zinapatikana kwa wingi na kugawiwa kwa wakulima nchini.

“Tunahitaji mbegu bora za pareto tani tatu ili zitumike kuzalisha tani 9,000 za pareto baada ya mwaka mmoja ambapo viwanda viko tayari kuinunua toka kwa wakulima” alisisitiza Bashe

Naibu Waziri huyo alizipongeza Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) ambayo itanunua tani 6,000 kwa mwaka huku kampuni ya TAN Extract Ltd ikihitaji tani 1,000 na kampuni ya PYTECH Ltd ikihitaji tani 2,000 za maua ya pareto itakayozalishwa na wakulima msimu wa 2022/23.

Katika hatua nyingine, Bashe alibainisha mikakati ya wizara kuhakikisha zao la pareto linakuwa na tija na uzalishaji wake unaongezeka zaidi ambapo alitaja mambo sita .

Kwanza kuongeza utafiti na uzalishaji wa mbegu bora tani 3 kupitia TARI, pili kuanzisha mfumo wa kilimo mkataba (Contract Farming), tatu kuanzisha mfumo wa ushirika kwa kuanzisha AMCOS za wakulima wa pareto.

Mkakati wa nne ni kuhamsisha Halmashauri kutenga mashamba vitalu kisha kugawa kwa wakulima na lengo ni kuanzia ekari 200.

Bashe alisema mkakati wa tano kusajili na kuwatambua wakulima wa pareto na sita wizara itaendelea na juhudi za kuondoa migogoro baina ya wanunuzi kwa kutenga kanda.

Mkulima bora wa zao la pareto, Anangisye Mwankina kutoka Kata ya Ipelele Kijiji cha Makwaranga Tarafa ya Magoma wilaya ya Makete, aliomba wizara kuwashirikisha viongozi wa wilaya nchini kutoa ushirikiano wa karibu kwa wakulima wa pareto ubora wa zao uongezeke hatua itakokuza bei.

Mwankina ambaye amekuwa mkulima bora wa pareto tangu mwaka 2014 hadi sasa, alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kwenda kutembelea wakulima wa Makete hatua itakayoongeza ari ya kilimo hicho.

Kwa mujibu wa Mwankina, analima ekari tatu na kwa mwaka huvuna kilogramu 800. “Tatizo tatizo letu benki zinatukopesha kwa riba kubwa mno hatua inayotukwamisha. Tufikishie salamu kwa Rais aje atutembelee,” alisema.

Mkurugenzi wa Bodi ya Pareto, Lucas Ayo alisema uzalishaji wa zao hilo umeongezeka kutoka tani 2,011 mwaka 2015/16 hadi kufikia tani 2,510 mwaka 2019/20 kati ya lengo la kuzalisha tani 3,000.

Alisema pia tija imeongezeka kutoka wastani wa kilogramu 250 kwa ekari mwaka 2015/16 hadi kufikia kilogramu 270 kwa ekari mwaka 2019/20.

Wastani wa bei ya chini anayolipwa mkulima imepanda kutoka Sh 1500 mwaka 2015/16 hadi Sh 2,400 mwaka 2019/20 na Sh 2,500 mwaka 2020/21 kwa kilo ya pareto.

Alitaja mkakati wa Bodi katika mwaka 2021/22 ni kuongeza utafiti wa kina kuhusu matumizi mbalim-

bali ya bidhaa za pareto ikiwemo visumbufu vya mimea mashambani, majumbani na kwenye maghala ya mazao hatua itakayochochea kukuza kilimo na tija cha zao la pareto.

Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza alisema wakulima jimboni mwake wanaomba wizara ifanye zao la pareto kuwa la kimkakati kwani ndilo linategemewa zaidi kimapato.

Kuhusu suala la kutenga maeneo ya kilimo, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga alisema wamelenga kuongeza eneo la uzalishaji pareto kutoka ekari 40 za sasa hadi kufikia ekari 100 kwa kutumia mfumo huo wa vitalu hatua itakayokuza uzalishaji. Msimu huu wamezalisha tani 4.3 za pareto .

Pareto inalimwa kwenye mikoa ya Arusha, Manyara, Songwe, Njombe na Iringa . Hadi Februari mwaka huu, Bodi imesajili wakulima 10,586 kwenye mfumo wake wa utambuzi na huduma kwa wakulima.

Join our Newsletter