Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 11Article 542200

xxxxxxxxxxx of Friday, 11 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kodi nafuu kwa wengi

SERIKALI imetangaza kufanya marekebisho ya kodi, ada, tozo na ushuru wa forodha kwenye huduma na bidhaa mbalimbali ikiwamo kodi ya majengo sasa itakuwa inatozwa kwenye manunuzi ya umeme kwa kila mwezi huku adhabu kwa makosa ya pikipiki na bodaboda ikipunguzwa kutoka Sh 30,000 hadi Sh 10,000.

Kabla ya mabadiliko hayo, kodi ya majengo ilikuwa ikitozwa kwa mwaka kwa Sh 10,000 kwa wenye nyumba za chini, za ghorofa Sh 50,000 lakini sasa kila mwezi kwa wenye nyumba za chini watatozwa Sh 1,000 kwa mwezi ambayo ni sawa na Sh 12,000 kwa mwaka na Sh 5,000 kwa kila ghorofa ambayo ni sawa na Sh 60,000 kwa mwaka.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alitangaza marekebisho hayo jana wakati akiwasilisha bungeni Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

“Napendekeza kodi ya majengo ya kiwango cha shilingi 1,000 kwa mwezi kwenye nyumba za kawaida zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme (LUKU).

“Aidha, napendekeza kiwango cha shilingi 5,000 kwa mwezi kwa kila ghorofa au apartment zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme (LUKU). Serikali itaweka utaratibu kwenye nyumba za kawaida na za ghorofa zinazochangia mita moja na zinazotumia mita zaidi ya moja,” alifafanua Dk Mwigulu.

Alisema ili kuondokana na tabia ya waendesha bodaboda kutelekeza pikipiki zao kwenye vituo vya polisi pindi wanaposindwa kulipa faini, adhabu zinazotolewa chini ya Sheria ya Usalama Barabarani imepunguzwa kutoka Sh 30,000 za sasa hadi Sh 10,000 kwa kosa moja.

Pia serikal imepunguza ada ya usajili ya magari kwa namba binafsi kutoka Sh milioni 10 hadi Sh milioni tano kila baada ya miaka mitatu.

Alisema serikali itaanzisha tozo ya ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye pikipiki zilizotumika kwa zaidi ya miaka mitatu zinazoingizwa nchini. “Lengo la marekebisho haya ni kudhibiti uingizaji wa pikipiki chakavu na kulinda mazingira. Hatua hii inatarajiwa kuongeza ya mapato ya serikali kwa Sh milioni 263.7,” alisema.

Aidha, alisema serikali imesamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye simu janja za mkononi, vishikwambi na modemu. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha matumizi ya huduma za mawasiliano ili kufikia lengo la asilimia 80 ya watumiaji wa intaneti ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 46 iliyopo sasa.

Maeneo mengine yaliyoguswa ni kupunguza ushuru wa bidhaa kwenye bia zinazotengenezwa kwa kutumia shayiri iliyozalishwa hapa nchini kutoka Sh 765 kwa lita za sasa hadi Sh 620 kwa lita na pia kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye matairi mapya ya pikipiki.

Alitaja marekebisho kwenye sheria ya ushuru wa barabara kwa kuongeza ushuru huo kwa Sh 100 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli na fedha hizo ziwe kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za vijijini kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Dk Mwigulu alitangaza kuongezwa tozo ya mafuta ya taa kutoka Sh 150 hadi Sh 250. Lengo la hatua hii ni kupunguza uchakachuaji wa mafuta kutokana na ongezeko la ushuru wa mafuta kwenye dizeli na petroli.

“Kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye siagi ya karanga, kupunguza Ushuru wa Forodha hadi asilimia sifuri kutoka viwango vya awali vya asilimia 10 na asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa vifaa maalumu vinavyotumika katika kupambana na ugonjwa wa homa kali

ya mapafu (Covid-19).

Vikiwemo barakoa, sanitizer, mashine za kusaidia kupumua na mavazi maalumu ya kujikinga yanayotumiwa na madaktari na wahudumu wa afya (PPE). Msamaha huu utatolewa kwa utaratibu wa “duty remission.” Hatua hii inalenga kutoa unafuu wa uzalishaji wa vifaa hivyo hapa nchini ili kuongeza kasi katika kupambana na ugonjwa huo,” alisema.

Alitaja kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mashine za kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya serikali (EFDs) pamoja na kupunguza ada za matangazo.

Kuhusu adhabu kwa mwajiri aliyeajiri raia ya kigeni, alisema “Kuweka adhabu ya shilingi 500,000 kwa kila mwezi kwa mwajiri aliyeajiri raia wa kigeni na kushindwa kuwasilisha ritani za kila mwezi zenye taarifa za raia wa kigeni aliowaajiri ikiwemo taarifa zao za mishahara kwa Kamishna wa Kazi. Lengo la pendekezo hili ni kuhimiza uwajibikaji wa hiari”.

Kuhusu Zanzibar alisema “Napendekeza kutekeleza utaratibu wa kuruhusu mapato yanayotokana na kodi na tozo za Muungano kwenye mapato yanayotokana na tozo za viza ili yaweze kutumika pale yalipokusanywa kama ilivyo kwenye mapato mengine ya Muungano.

“Mapendekezo haya yanafanya suala hili liondolewe kwenye orodha ya changamoto za Muuungano. Mapato yatokanayo na tozo za Viza upande wa Zanzibar yaonekane kwenye bajeti upande wa Zanzibar, kuidhinishwa na kutumika Zanzibar.”

Alitangaza pia kufanya marekebisho kurudisha utaratibu wa kurejesha VAT kwa bidhaa zinazonunuliwa Tanzania Bara na kutumika Tanzania Zanzibar.

“Hii inatokana na mfumo wa kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri kwa bidhaa za viwandani pekee kutowanufaisha wafanyabiashara wa Zanzibar wanaonunua bidhaa na kutozwa VAT Tanzania Bara na kutozwa tena VAT bidhaa hizo zinapopelekwa Zanzibar,” alieleza.

Aidha, alisema inapendekezwa marejesho ya VAT yatakayofanyika kwa bidhaa zinazotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar yafanyike pia kwa bidhaa zitakazotoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara sambamba na marekebisho ya vifungu husika vya sheria za VAT kwa pande zote mbili za Muungano.

“Ili kuwa na ufanisi wa marejesho, maboresho ya mifumo yatafanyika ili isomane baina ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kutokana na utaratibu huu, kiwango cha asilimia sifuri ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kilichokuwa kinatozwa bidhaa hizo kitasitishwa,” alieleza.

Pia serikali imepunguza tozo kutoka asilimia 2.5 hadi asilimia 0.5 kwa umiliki mpya wa ardhi; kupunguza tozo kutoka asilimia moja hadi asilimia 0.5 kwa urasimishaji.

Dk Mwigulu alisema kuanzia Julai mwaka huu serikali itatoza tozo ya Sh 10 hadi Sh 10,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa. Kiasi cha tozo kinatofautiana kulingana na thamani ya muamala wa fedha unaotumwa au kutolewa. Pendekezo hili litaongeza mapato ya serikali Sh milioni 1,254,406.14.

Pia kutoza Sh 10 hadi Sh 200 kwa siku kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa watumiaji. Pendekezo hili litaongeza mapato ya serikali ya Sh milioni 396,306.

Join our Newsletter