Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 03Article 540667

xxxxxxxxxxx of Thursday, 3 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

‘Kugawanywa kwa Selous  hakutaathiri utalii Tawa’ 

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema kugawanywa kwa pori la akiba la Selous na kuanzishwa kwa Hifadhi ya Nyerere hakutathiri shughuli za utalii katika maeneo yake.

Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo, Mabula Nyanda alisema jana kuwa, Tawa imetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa kitalii ili kuongeza uwezo wa kifedha katika kusimamia maeneo yaliyo chini ya mamlaka hiyo, ikiwa ni moja ya mkakati wa ukuzaji na uendelezaji wa mamlaka na kuongeza pata la taifa.

Nyanda alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Morogoro.

Alisema wameandaa mipango ya usimamizi ya utalii ili kuongeza watalii ikiwa ni pamoja na kuunganisha na maeneo mengine katika kutangaza vivutio kwa Watanzania na wageni.

Alitaja maeneo hayo ya hifadhi kuwa ni pamoja na hifadhi ya Mpanga-Kipengere, hifadhi ya Pande, hifadhi ya Mkungunero, hifadhi ya Kijershi, hifadhi ya Swangaswanga na eneo la urithi wa dunia la Kilwa.

Nyanda alifafanua kwamba kayika eneo la urithi wa dunia la Kilwa kumetengwa maeneo matatu kwa ajili ya uwekezaji ambayo ni Kilwa Kisiwani, Songo Mnara na Sanje Kati.

Alisema kutokana na jitihada zinazofanywa na Tawa mapori ya akiba yamezidi kuvutia watalii.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamishna huyo alisema katika kipindi cha mwaka 2015/2016 watalii 35,479 kutoka mataifa mbalimbali walitembelea mapori ya akiba na kwa mwaka 2018/2019 watalii 129,428 walikwenda kwenye maeneo hayo.

Alitoa mwito kwa Watanzania kuwekeza katika ufugaji wa wanyamapori kupitia bustani za wanyamapori, mashamba na ranchi za wanyamapori.

Kwa mujibu wa Nyanda hadi sasa vitalu 28 vimetengwa kwa ajili ya uwekezaji kupitia biashara ya uwindaji wa kitalii.

Join our Newsletter