Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 07Article 541432

Habari za Afya of Monday, 7 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kula chakula salama leo kwa afya njema kesho

Kula chakula salama  leo kwa afya njema kesho Kula chakula salama leo kwa afya njema kesho

DUNIANI kote hakuna nchi ambayo inaweza kufujifungia mipaka yake ikasema inajitosheleza yenyewe kwa chakula inachokizalisha. Kwa lugha nyingine, kila nchi inategemea kupata chakula kutoka nchi nyingine.

Hata pale watu wanaposafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine wanatakiwa kupata chakula salama kama kilivyo chakula cha asili cha nchi wanakotoka.

Kwa kutambua hilo, mwaka 2018 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipitisha Azimio Na. 73/250 kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Usalama wa Uchakula Dunia.

Azimio hilo lilipitishwa na WHO kwa lengo kusimamia na kudhibiti masuala ya usalama wa chakula, hivyo ni lazima chakula kiwe salama hata kinaposafirishwa kwenda nchi nyingine.

Azimio hilo lilianza kutekelezwa mwaka 2019, ambapo Juni 7, mwaka huo maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Usalama wa Chakula Duniani yalianza mwaka 2019 na mwaka huu yanafanyika kwa mara ya tatu.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, leo ikikiwa ni kilele chake, WHO imetoa kaulimbiu ambayo Tanzania kama nchi mwanachama inaitumia pia ikiwa na ujumbe usemao: "Chakula salama sasa kwa afya njema kesho."

Ofisa Usalama wa Chakula Darasa la Kwanza katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Kaiza Kilango, anasema pamoja na kaulimbiu hiyo, kuna ujumbe mdogo mdogo unaotumika kwenye maadhimisho hayo.

Miongoni mwa ujumbe huo ni ule usemao; "Hakuna uhakika wa chakula kama chakula sio salama."

Kwa mujibu wa Kilango, hiyo ina maana kwamba kwenye uhakika wa chakula wanalenga mambo makuu manne, la kwanza likiwa ni upatikanaji wa chakula, pili chakula kufikiwa na wahitaji, tatu usalama wa chakula na nne chakula kuwa lishe bora.

Kwa mujibu wa Kilango katika vitu hivyo vinne vinavyotengeneza uhakika wa chakula, ikitokea tu usalama wa chakula ukawa na shida, vyote vinakuwa ni sawa na bure.

"Hata tukipata chakula na kikawa na viini lishe, lakini kikawa sio salama, badala ya kupata faida tunayotarajia, haitapatikana na matokeo yake tutaishia kuugua," anasema Kilango.

Anataja ujumbe wa pili mdogo kwenye kaulimbiu ya mwaka huu ni; "Chakula ni hitaji la msingi kwa afya na ustawi wa jamii."

Kwa mujibu wa Kilango, WHO kwenye ripoti yake ya mwisho ya masuala ya chakula ambayo ilitolewa mwaka 2010 inaeleza kwamba duniani kote inakadiriwa watu milioni 600 wanaugua kila mwaka kutokana na kula chakula kisichokuwa salama.

Kati ya hao, anasema watu 420,000 wanapoteza maisha kwa mwaka kutokana na kula chakula kisicho salama. Kwa mujibu Kilango, takwimu hizo zinapatikana katika nchi zenye mifumo imara ya ukusanyaji wa takwimu.

"Kwa hiyo bado kuna nchi ambazo mifumo yake ya ukusanyaji takwimu sio mzuri sana kuweza kupata kila takwimu ya madhara yatokanayo na chakula," anasema Kilango.

Anatoa mfano kwamba kuna wakati watu wakienda kwenye harusi leo, kesho yake utawasikia wakisema chakula kile hakikuwa kizuri, wakidai kuumwa matumbo. Wakiulizwa kama wameenda hospitali, wanasema walinunua dawa maana yake hapo hiyo takwimu inakuwa imepotea.

"Pale watu wanapokosa mwitikio mzuri wa kwenda hospitali maana yake nchi inapoteza takwimu. Kwa maana hiyo takwimu hizo za watu milioni 600 kuugua kutokana na matumizi ya chakula kisicho salama kidunia bado hazitoi picha halisi kutokana na mifumo yetu ya ukusanyaji takwimu," anasema Kilango.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, hiyo inaonesha kwamba ipo shida kwenye masuala ya usalama wa chakula, kwani watu 420,000 kupoteza maisha kila mwaka kutoka na kukosekana kwa usalama wa chakula, sio jambo la kupuuzia.

Hivyo, anasema maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kukumbushana kila mtu, kama nchi, serikali na taasisi kuzingatia usalama wa chakula.

"Mfano, wamiliki wa shule wanatakiwa kujua chakula wanachokinunua kwa ajili ya wanafunzi wanakinunua wapi, wanakihifadhi wapi ili kisiweze kusababisha matatizo ya afya kwa wanaokitumia.

Vivyo hivyo hata kwenye taasisi nyingine kama kwenye magereza na hiyo inaenda hadi kwenye kaya. Mzazi ana jukumu la kuhakikisha chakula ni salama."

Anafafanua kwamba ndiyo maana serikali imeweka mifumo mbalimbali ya kuhakikisha chakula kinakuwa salama hata kinachopatikana kwenye mifugo, ndiyo maana imeweka utaratibu wa mifugo kuchinjiwa kwenye machinjio yanayokaguliwa.

"Hivyo unaweza kukuta bei ya nyama inayouzwa kutoka kwenye machinjio yanayotambulika ni shilingi 6,500 kwa kilo, lakini wakati mwingine ukakuta kuna nyama inauza shilingi 4,500 sehemu fulani, hapo ni lazima hiyo iingie kwenye kichwa chako kwa nini huyu ameshusha bei hivi!

Ukiwa mdadisi unaweza kujua kwamba pengine kuna bucha mitaani inachinja ng'ombe bila kukaguliwa, kwa hiyo kila mtu ana wajibu wa kusimamia usalama wa chakula badala ya kusema kila kitu kitafanywa na serikali," anasema Kilango na kuongeza kwamba chakula kinaweza kuchafuliwa na bakteria, minyoo au sumu.

Kuhusu mikakati ya shirika katika kuhakikisha watu wanakula chakula salama, Kilango anasema TBS inaandaa viwango ambavyo vinatakiwa kufikiwa na kuzingatiwa na kila mzalishaji.

Anaongeza kuwa chakula pia kinaandaliwa kwa viwango, lakini kuna vyakula ambavyo vinasindikwa.

"Kwa hiyo tunakwenda kumkagua mzalishaji ili kujiridhisha wapi anapata malighafi, mfumo wake wa ukusanyaji malighafi ukoje, lakini pale anapozalisha ana wataalamu? Hiyo ni kazi yetu," anasema na kuongeza:

"Ni lazima tujiridhishe kama anafanyakazi zake kwa kuzingatia viwango? hivyo hapo tutachukua sampuli kwa ajili ya kwenda kuzipima kwenye maabara zetu, kwa sababu viwango kwenye chakula ni hitaji la lazima."

Wakishapima sampuli za bidhaa za mzalishaji na kukidhi vigezo, anasajiliwa na chakula chake kinapata nembo ya ubora na baada ya hapo sehemu ya uzalishaji wake inakuwa ikitembelewa na maofisa wa TBS mara tatu hadi nne kwa mwaka bila yeye kujua.

"Kadri anaposhindwa kufikia matakwa ya viwango aliyopewa, ndivyo tunaongeza idadi muda wa kutembelea na kumfanyia ukaguzi ili kuhakikisha uzalishaji wake unakidhi vigezo vya ubora na usalama," anasema.

Aidha, anasema wanao mfumo mwingine wa kupita madukani, ambapo shirika kwa kutumia wakaguzi wake wanapewa fedha, hivyo wanaingia sokoni na kununua bidhaa za aina mbalimbali kama wateja wa kawaida.

"Bidhaa zote ambazo tulishazipima huko nyuma na kusema kiwanda fulani kinazalisha bidhaa bora na salama tunazinunua madukani na kwenda kuzipima kwenye maabara zetu.

Kwa hiyo pamoja na kwenda kufanya ukagua katika sehemu yake ya uzalishaji, tununua bidhaa zake sokoni na kwenda kuzipima bila yeye kujua, ili kujiridhisha kama bidhaa zake zipo vizuri," anasisitiza.

Anasema pale wanapobaini kuna shida wanarudi tena kiwandani kwake kwa ajili ya kufanya ukaguzi.

"Kwa vyakula ambavyo havipiti viwandani, bali vinaenda moja kwa moja kwenye soko kama vile nyanya, mahindi au kabeji, huko wataalamu wa TBS kwa kushirikiana na wataalamu wengine wa serikali nako wanatembelea," anasema.

Anafafanua kwamba wamekuwa wakifanya ufuatiliaji mashambani, kufanya mikutano na maofisa kilimo ili kuwataka wahakikishe wanazingatia kanuni bora za kilimo na matumizi sahihi ya dawa zinazotumiwa shambani.

Mbali na hiyo wanakwenda mbali zaidi na kuchukua bidhaa na kuzipima zikiwemo nafaka kama mahindi.

Mtaalamu huyo anatoa wito kwa wananchi kuhakikisha chochote wanachotaka kula, kujiuliza kwanza wanapeleka nini kwenye tumbo lao.

"Hata mkulima anapotaka kuweka dawa kwenye shamba lake, lazima akumbuke hicho ni chakula, hivyo lazima azingatie ushauri wa watalaam," anasema Kilango.

Kwa mujibu wa Kilango kuwekeza kwenye masuala ya usalama ya chakula kama nchi kuna faida ya sasa na baadaye.

Anatoa mfano, akisema Tanzania kama nchi inapata mvua ya kutosha kwa mwaka na mito mingi, hivyo ni fursa nzuri ya kupata soko la chakula kwa nchi ambazo hazina usalama wa kutosha kama vile Somalia, Sudan.

"Hatufurahii hali wanayokuwa nayo wenzetu wa Sudan na Somalia, lakini kama nchi wakati mwingine inatupa fursa ya kupeleka chakula kule, kwa hiyo kama nchi na wananchi wake wafahamu kwamba tumebarikiwa kuwa na nchi yenye mito, mvua ya kutosha na udogo wenye rutuba, hivyo lazima wajue tunapolima tutapata chakula kingine ambacho hatuwezi kukimaliza, tutahitaji kukiuza,"anasema na kuongeza;

"Ili chakula hicho kiende nje ni lazima kitapimwa ili kionekane kinakidhi vigezo vya usalama, kwa hiyo tukiwekeza katika hilo vyakula vyetu vitakuwa fursa kubwa ya kibiashara.

Anasema katika hilo, serikali kwa nafasi yake iafanyakazi kubwa ya kusomesha wataalam wa kutoa elimu kwa wananchi, hivyo kila mdau atimize wajibu wake ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula salama.

Join our Newsletter