Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 09Article 584422

Habari Kuu of Sunday, 9 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Kutokuwepo kwa chaguo la pili sekondari ni muujiza?

Kutokuwepo kwa chaguo la pili sekondari nimuujiza? Kutokuwepo kwa chaguo la pili sekondari nimuujiza?

Kitendo cha mwaka huu kutokuwapo machaguo mawili ya wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza, kimeendelea kupongezwa na wadau wa elimu wakiutaja kuwa ni muujiza uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Pongezi hizo zimekuwa zikitolewa na watu wa kada tofauti kutoka maeneo mbalimbali ya nchi baada ya kushuhudia kasi ya ujenzi wa madarasa ambao umetoa fursa kwa wanafunzi wengi kuanza masomo ya sekondari mwaka huu.

Miongoni mwa wadau hao ni Mwalimu Mstaafu, Juliana Ndahani aliyesema juzi kwamba, katika utumishi wake akiwa mwalimu kwenye shule za msingi, sekondari na kisha vyuo vya ualimu, hakuwahi kuona mwaka ambao wanafunzi wote wanajiunga kidato cha kwanza bila awamu.

Alisema hayo juzi katika Shule ya Sekondari Chamwino wakati Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka akitembelea madarasa ya shule za sekondari zilizojengwa kwa fedha za Covid-19. “Huu ni muujiza…Kwa mara ya kwanza wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaanza shule wakiwa pamoja na kukiwa hakuna chaguo la kwanza na la pili katika kupangiwa shule,” alisema Ndahani.

Mwalimu huyo aliyehudumu serikalini kwa miaka 40, alisema miaka yote akiwa mwalimu, kulikuwa na chaguo la kwanza na la pili la wanafunzi kujiunga sekondari, hali ambayo ilikuwa ikipunguza ufanisi kwa wanafunzi kwani walikuwa wanaingia kidato cha kwanza kwa nyakati tofauti.

Alisema pia wanafunzi wengi waliokuwa wakisubiri chaguo la pili walikuwa wakijikuta wakipotelea mitaani baada ya kukosa chaguo la kwanza. “Rais Samia amefanya maajabu,” alisema mwalimu huyo na kumuomba Mtaka aache alama ya elimu Dodoma kama alivyofanya mkoani Simiyu.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Chamwino, Namga Cleopa alisema walipata Sh milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ofisi moja ya walimu. Pia alipongeza hatua hiyo ya serikali kujenga madarasa. Shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha sita, ina wanafunzi 1,186. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka alisema Wilaya ya Chamwino imepata Sh bilioni 2.92 na kuwa fedha hizo zilizotolewa na serikali ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 146, shule shikizi zikiwa 64 na shule za sekondari zikiwa nane.

Alisema shule hiyo yenye eneo la ukubwa wa ekari 150 inaweza kuweka mipango ya kuwa na ujenzi wa shule ya mfano ambayo itachukua wanafunzi wenye vipaji.

“Mfikirie kujenga shule ya mfano na pia mfikirie kupanda miti ya matunda… yaani kila mtoto apande mti wake wa matunda,” alisema na kuongeza kuwa kazi imefanyika na inaonekana kama ambavyo Rais alitaka shida ya madarasa iishe.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk Fatma Mganga alisema katika mikoa mitano iliyopata fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, Dodoma imo. Alisema watendaji wamejitahidi katika kusimamia.

Alisema shule hiyo ina ekari 150, hivyo wanaweza kutumia sehemu ya eneo hilo kwa ajili ya uzalishaji wa chakula. “Tumieni hizo ekari vizuri kwa ajili ya kuzalisha chakula cha shule, watoto wafundishwe elimu ya kujitegemea, wafundishwe kilimo cha kujitegemea wakiwa shuleni," alisema na kuongeza kuwa mkoa huo umekuwa haufanyi vizuri kwa vile watoto wamekuwa hawapati chakula shuleni. Ofisa Elimu Sayansikimu na Mazingira Wilaya ya Chamwino, Sista Donasiana Nju alisema kwa baadhi ya shule wameanzisha kilimo cha mbogamboga na kuanzisha kilimo cha matunda kwa maeneo yaliyo na maji. Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Gift Msuya alisema walipata Sh bilioni 2.9 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.