Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 17Article 551986

Habari Kuu of Tuesday, 17 August 2021

Chanzo: ippmedia.com

LHRC, Jamhuri vuta nikute kesi ya "Tozo za Miamala"

WAKILI wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata, WAKILI wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata,

WAKILI wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata, amewasilisha pingamizi katika kesi ya kupinga tozo za miamala ya fedha na ametoa sababu tatu akidai shauri hilo halina msingi, hivyo lifutwe.

Pingamizi hilo liliwasilishwa jana Mahakama Kuu mbele ya Jaji John Mgeta wakati shauri lililofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lilipokuwa linasikilizwa.

Akiwasilisha pingamizi alidai maombi hayana msingi kwa sababu hakuna uamuzi wowote uliotolewa na walalamikiwa, ambao unahitaji kufutwa na mahakama, walichofanya walalamikiwa ni kutimiza wajibu wao kikatiba kutafuta chanzo cha mapato.

Sababu ya pili alidai maombi hayana msingi kwa sababu yaliwasilishwa na taasisi bila kuwa na maamuzi ya bodi, wakati kisheria taasisi inapotaka kufungua shauri ni lazima kuwapo na maamuzi ya kutoka kwenye bodi.

"Katika shauri hili hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba bodi iliidhinisha kufunguliwa kwa shauri, huyo Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Anna Henga, alipaswa kufungua mwenyewe na siyo kupitia kituo," alidai Wakili Malata.

Wakili Malata alidai mlalamikaji hajaonyesha namna gani anavyoathirika na hakuonyesha anaathirika vipi na wala hakuonyesha maslahi yake.

Akijibu Wakili Mpale Mpoki alidai sheria inaruhusu ikiwamo ile iliyoanzisha tozo kupingwa mahakamani.

Alidai hoja kuhusu uamuzi wa bodi siyo pingamizi la kisheria kwa sababu ni suala linalohitaji ushahidi na kwamba aliyeapa katika kiapo kuonyesha dalili kwa namna gani kaathirika na alifanya hivyo kwa niaba ya umma na ana maslahi katika shauri hilo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 8, 2021, ambapo Mahakama itatoa uamuzi.

Katika shauri hilo, LHRC inaomba mahakama ifanye mapitio kuhusu sheria ya mfumo wa taifa wa malipo pamoja na kanuni zake zilizoweka tozo katika miamala ya fedha kwa njia ya simu.

Shauri hilo lilitokana na kupitishwa kwa mapendekezo ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021 na sheria ya fedha iliyosababisha kuweka tozo ambayo anaitaja kuwa mzigo kwa wananchi wa kawaida na wafanyabiashara ndogo ndogo.