Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 31Article 554572

Siasa of Tuesday, 31 August 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Lembeli kuwania Ubunge Jimbo la Kwandikwa

James Lembeni, aliyekuwa mbunge wa Kahama James Lembeni, aliyekuwa mbunge wa Kahama

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kahama, James Lembeli amejitosa kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea Jimbo la Ushetu katika Ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Elias Kwandikwa kufariki dunia.

Lembeli alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kahama kwa muda wa vipindi viwili kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 wakati huo Jimbo la Kahama na Ushetu lilikuwa moja kabla ya kuligawa na kupatikana Jimbo la Ushetu.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu leo Jumanne Agosti 31, 2021 Lembeli amesema kuwa endapo chama kitamapatia ridhaa ya kugombea jimbo hilo atahakikisha anayatekeleza yale aliyoyaacha Kwandikwa hasa katika sekta ya afya, elimu, kilimo, miundombinu ya barabara pamoja na huduma ya maji.

Amesema kuna baadhi ya watu wanasema kuwa alilikimbia jimbo hilo katika uchaguzi wa mwaka 2015 na kugombea Jimbo la Kahama jambo ambalo sio kweli na kwamba alifanya hivyo kumwacha Kwandikwa achukue jimbo hilo.

Lembeli amesema yeye ndiye aliyemtambulisha Kwandikwa wakati akitia nia ya kugombea katika jimbo hilo katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Igunda kwa mara kwanza na kwamba ndio maana aliamua kugombea katika Jimbo la Kahama katika kipindi hicho.

“Nimeamua kuchukua fomu hii kwa lengo la kuyaendeleza yale ambayo marehemu Kwandikwa alikuwa akiyafanya jimboni kwa kipindi cha uhai wake, nitaelekeza nguvu zaidi katika kutatua changamoto ya nishati ya umeme, vituo vya afya, maji na miundombinu ya barabara,”alisema Lembeli.

Hata hivyo, Lembeli alisema kuwa anasikitika kwa taarifa za uchukuaji wa fomu hizo kutolewa mapema na baadhi yao walikuwa hawafahamu kama zoezi hilo linaendelea huku muda ukiwa ni mdogo wa kujaza na kurudisha fomu hizo.

“Mimi nilisikia usiku kuwa tayari tumeruhusiwa kuchukua fomu hizo za kugombea ndio maana hata mimi nimekuja asubuhi hii bila ya kuwa hata na sare za chama, hatuna budi kuendelea kupambana kuhakikisha kuwa jimbo hilo ninaliongoza kwa mara nyingine,” aliongeza Lembeli.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CCM wilayani Kahama, Emanuely Mbamange jana alitoa taarifa kwa vyombo vya habari ya jimbo la uchaguzi la Ushetu lipo wazi na wagombea wanaruhusiwa kufika katika ofisi za chama hicho kwa ajili ya kuchukua fomu.