Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 03Article 540661

xxxxxxxxxxx of Thursday, 3 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Lukuvi afuta waraka kuhusu madiwani

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amefuta waraka namba moja unaowaondoa madiwani kushiriki katika shughuli za uidhinishaji mipango ya uendelezaji miji katika maeneo yao uliotolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi nchini.

Kabla ya kutolewa waraka huo mpya, madiwani kupitia kamati zao za mipango miji walikuwa ndio wenye mamlaka ya kubariki mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri husika kupitia vikao vyao vya robo mwaka na waraka mpya unataka shughuli hizo sasa kufanywa na wataalamu wa mipango miji kwa kushirikisha sekta mbalimbali kama vile sekta za maji, barabara, umeme.

Lukuvi alifanya uamuzi huo akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru alipongumza na madiwani wa halmashauri hiyo katika ziara ya kusikiliza na kutatua kero za ardhi katika Mkoa wa Arusha.

Alisema sasa waraka huo ameufuta mpaka utakapotolewa mwingine wenye maelekezo yenye tija.

Lukuvi alisema haiwezekani kuwaondoa madiwani kupitisha mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri zake kwa kuwa mamlaka ya upangaji bado ziko chini ya halmashauri.

"Nimeamua kuufuta waraka namba moja unaokataza madiwani kupanga mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri zenu, huwezi kuwa na halmashauri inayoshindwa kupitisha au kubariki mipango ya wilaya katika matumizi ya ardhi," alisema.

Kwa mujibu wa Lukuvi, wataalamu wa mipango miji katika ofisi za ardhi za mikoa waendelee kuwa washauri kwa kamati za mipango miji katika mabaraza ya madiwani.

"Kama vibali vya ujenzi tuliwaondoa na kupanga pia tuwaondoe, mtafanya kazi gani? Hiyo haiwezekani, kwa sasa mwongozo unaokuja kamati za ardhi na makazi zitapatiwa ufafanuzi wa namna bora ya matumizi ya ardhi na baadaye kupelekwa kwa maofisa mipango miji,” alisema.

Katika hatua nyingine, Lukuvi ametangaza kufutwa kwa shamba la Valeska lenye ukubwa wa ekari 4,087 katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru mkoani Arusha.

Alitangaza uamuzi huo baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufuta shamba hilo kutokana na kuombwa kufanya hivyo na waziri wa ardhi.

Lukuvi alisema Halmashauri ya Wilaya ya Meru itawajibika kulipa fidia katika maeneo yanayohitaji fidia ambapo kwa mara ya mwisho fidia ilikuwa Sh milioni 394.10.

Lukuvi alianisha matumizi ya shamba lililofutwa kuwa ni ekari 1,500 kugawiwa kwa vijiji vitatu vya Kwaugoro, Valeska na Maloloni.

Alisema ekari 1,028 zitatumika kwa shughuli za kilimo na ekari 1,559 kwa matumizi mbalimbali kama makazi na biashara.

Join our Newsletter