Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 25Article 544150

Habari Kuu of Friday, 25 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

MCT yamlilia Mkinga

MCT yamlilia Mkinga MCT yamlilia Mkinga

BARAZA la Habari Tanzania (MCT), limeshtushwa na taarifa za kifo cha ghafla cha Mhariri Mkuu wa gazeti la Jamhuri, Mkinga Mkinga, kilichotokea leo Juni 24, 2021 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutokana na maradhi ya shinikizo la damu.

Taarifa ya MCT iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Kajubi Mukajanga imesema kuwa Mkinga aliugua ghafla siku ya Jumapili, Juni 20, 2021 na kupelekwa katika Hospitali ya Kitengule, iliyopo jijini Dar es Salaam, ambapo taarifa kutoka kwa madaktari zilisema kuwa alipata tatizo la mishipa ya kichwani na hivyo kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

“Baraza litamkumbuka marehemu Mkinga kwa jitihada zake za kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi kwa weledi na umahiri mkubwa. Wakati wa uhai wake marehemu alipigania kitu alichokiamini na kuhakikisha kinatimia,” amesema Mukajanga.

Amesema Mkinga alikuwa ni mmoja wa waandishi wachache wanaoandika habari za uchunguzi hapa nchini na kwamba tasnia imempoteza mwana habari mahiri na Baraza litaendelea kumkumbuka daima.

“Tunachukua fursa hii kutoa pole za dhati kwa familia ya marehemu, wanatasnia ya habari, ndugu na jamaa wote kwa kufikwa na msiba huo mzito,” amesema.

Wakati wa uhai wake, Mkinga aliwahi kuwa mshindi wa jumla wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2014, ambapo katika shughuli hizo, mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais Mstaafu, Ghalib Bilal.