Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 10Article 542026

xxxxxxxxxxx of Thursday, 10 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ma-DED wabanwa ukusanyaji mapato

WAKURUGENZI wa halmashauri 8 za Mkoa wa Tabora wametakiwa kuongeza kasi na weledi katika ukusanyaji mapato ili kuhakikisha wanafikia malengo yaliyowekwa na serikali.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa huo Ali Hapi katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi mjini hapa alipokuwa akizungumza na viongozi wa serikali wakiwemo wakuu wa wilaya, wakurungenzi ,makatibu tawala wa wilaya, wataalamu na viongozi wa madhehebu ya dini.

Alisema mkoa huo umejaliwa kuwa na rasilimali na vyanzo vingi vya mapato hivyo akawataka wakurugenzi, wataalamu na watendaji walioko katika halmashauri hizo kusimamia ipasavyo ukusanyaji mapato na kubuni vyanzo vipya.

Aliongeza kuwa mkoa huo wenye takribani watu milioni 3 umejaliwa pia kuwa na ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali na mifugo mingi lakini bado haufanya vizuri hivyo akawataka kuongeza juhudi zaidi ya usimamizi.

“Kama niliweza kukusanya sh bil 20 za mapato katika Mkoa wa Iringa ambao ni mdogo kwa nini Tabora ishindikane, nataka tuongeze juhudi na kasi zaidi ili kuongeza mapato”, alisema.

Hapi alibainisha kuwa hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu Mkoa huo ulikuwa umekusanya asilimia 59 tu na umebaki mwezi 1 kumaliza mwaka wa fedha, hivyo akaagiza kila halmashauri kuhakikisha inafikia malengo.

Aidha aliwataka Viongozi na Watumishi wa halmashauri zote za Mkoa huo kushikamana na kuchapa kazi kwa bidii huku aki-

wataka kujiepusha na tabia za majungu kwa kuwa hayajengi, bali hurudisha nyuma maendeleo.

Mkuu huyo aliagiza watumishi kwenda kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi ili kupunguza mlundikano wa mashauri yanayopelekwa mahakamani kwani mengi husababishwa na viongozi kutokuwa karibu na jamii.

Join our Newsletter