Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 22Article 573583

Habari Kuu of Monday, 22 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Maagizo ya DPP kuhusu jalada la walioghushi cheti cha ndoa

Maagizo ya DPP kuhusu jalada la walioghushi cheti cha ndoa Maagizo ya DPP kuhusu jalada la walioghushi cheti cha ndoa

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP) ameitisha ofisini kwake jalada la kesi ya kughushi cheti cha ndoa inayomkabili Khairoon Jandu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kesi hiyo iliyotakiwa kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Joseph Luambano.

Wakili wa utetezi, Abubakar Salim mara kadhaa alikuwa hafiki mahakamani kwa ajili ya kesi kuendelea na DPP aliamua kuliitisha jalada la kesi hiyo ofisini kwake.

Kesi hiyo ambayo upelelezi wake ulishakamilika muda mrefu na mashahidi kuandaliwa kwa ajili ya kuanza kutoa ushahidi wao, ilikwama mara kadhaa na kuahirishwa mpaka Novemba 29, mwaka huu ili kuangalia kama DPP atakuwa amerejesha jalada la kesi hiyo mahakamani hapo ama la.

Awali, kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa kwa mfululizo kuanzia Novemba 1 hadi 3, mwaka huu na miongoni mwa mashahidi ni wakili wa kujitegemea, Jerome Msemwa.

Awali, kabla ya jalada la kesi hilo kuitishwa kwa DPP ilikwama kuanza kusikilizwa kwa sababu Wakili wa Utetezi, Salim alikuwa anahudhuria kesi Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.

Baada ya taarifa hiyo Wakili wa Serikali Ashura Mzava alimlalamikia wakili huyo wa utetezi akidai ni mara ya tano sasa kesi hiyo inashindwa kuendelea kutokana na yeye kutofika mahakamani.

“Mheshimiwa hakimu pamoja na wakili kuleta taarifa hii, lakini naona kuna mchezo anafanya hii ni mara ya tano sasa kesi inashindwa kuendelea kwa yeye kutofika mahakamani, naandaa mashahidi lakini wakili haonekani mahakamani," alidai wakili Mzava.

Katika kesi hiyo Khairoon anadaiwa katika tarehe na mwezi usiofahamika mwaka 2020, jijini Dar es Salaam kwa njia ya udanganyifu alighushi cheti cha kuzaliwa cha mtoto Gurditsing Jandu, akionyesha kuwa kimetolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) wakati akijua kuwa ni uongo.

Katika shtaka lingine, Khairoon anadaiwa kuwa katika tarehe na mwezi usiofahamika mwaka 2020 alighushi cheti cha ndoa akionyesha kimetolewa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania Bakwata jambo alilojua kuwa sio kweli.