Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 10Article 556774

Habari za Afya of Friday, 10 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Maagizo yaliyotolewa leo na Waziri wa Afya kwa idara ya maendeleo ya jamii

Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya

Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu kuunda Kamati maalum itakayofanya tathimini ya mtawanyiko na mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa.

Dkt.Gwajima ametoa agizo hilo Leo septemba 10 mwaka 2021, jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya maazimio ya kikao cha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kilichofanyika Januari, 2021 na kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Serikali na Mashirika hayo ili kuleta Maendeleo endelevu ya Taifa kwa ujumla.

Agizo hili limekuja kutokana na maazimio na mapendekezo ya Mashirika hayo kwa Serikali ya kufanya tathmini ya mchango wa Mashirika hayo katika kuleta maendeleo kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwa na taarifa sahihi za Mashirika yapi yamefanya nini katika eneo gani.

Waziri Gwajima ameongeza kuwa Wizara itahakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili yaweze kusaidiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali.

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira ya kushirikiana na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuwaletea maendeleo wananchi katika Maeneo mbalimbali" alisema.

Aidha ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuzingatia uwazi na uwajibikaji kwa kuhakikisha fedha wanazozipokea kutoka chanzo mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi zitumike kwa kadri ilivyotarajiwa ili kuleta matokeo chanja katika jamii.