Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 22Article 559081

Dini of Wednesday, 22 September 2021

Chanzo: Mwananchi

Maaskofu na Wachungaji wa Anglikana Tanzania wakutana Dodoma

Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Mchungaji Can Dk Mecka Ogunde. Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Mchungaji Can Dk Mecka Ogunde.

Wachungaji 2,045 wa Kanisa la Anglikana Tanzania watashiriki Kongamano la pamoja Jijini Dodoma ambalo linakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya kanisa tangu liliposajiliwa nchini.

Kuanzia leo Septemba 22, 2021 wachungaji na Maaskofu wa Kanisa hilo wataanza kuingia Dodoma kutoka sehemu mbalimbali nchini kwa ajili ya kuanza vikao lakini mkutano wao utaanza rasmi Septemba 24,2021 katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha St John’s ambacho kinamilikiwa na kanisa hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Septemba 22,2021, Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mchungaji Canon Dk Mecka Ogunde amesema kongamano hilo litakuwa na maana kubwa kwa ajili ya kujadili mipango na maendeleo ya Kanisa na Tanzania.

Dk Ogunde amesema kusanyiko hilo litaongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Dk Maimbo Mndolwa kwa kusaidiana na Askofu msaidizi wa Jimbo Dk Dickson Chilongani na maaskofu wengine.

Katibu amesema Dayosisi 28 za Kanisa zitapeleka wachungaji wao, maaskofu na wajumbe wengine ambao watakuwa katika orodha hivyo wanaamini kutakuwa na ugeni mkubwa katika siku hivi kwa kanisa na mji wa Dodoma.

“Kilele cha Kongamano itakuwa ni Septemba 27 ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Samia Suluhu Hassan na amethibitisha kuwa atakuja siku hiyo, kwa hiyo tunaamini kila jambo litaendelea kwa Baraka zake Mungu,” amesema Dk Ogunde.

Amewataka wachungaji kutoka mikoa ya mbali ambao hawajaanza safari kujiandaa na kufika Dodoma kwa muda kama wlaivyokubaliana ili kwa pamoja wajiwekee malengo ya kwenda mbele zaidi kwa umoja na mshikamano wa kimaendeleo.