Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 29Article 560431

Diasporian News of Wednesday, 29 September 2021

Chanzo: Mwananchi

Maaskofu wamuangukia Dk Mwinyi kuhusu amani Zanzibar

Rais wa Zanzibar,  Dk Hussein Mwinyi Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

Baraza la maaskofu Zanzibar limemueleza Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi changamoto zinazolikumba kanisa ili azipatie ufumbuzi, wakisema zinaweza kusababisha migongano isiyo ya lazima na kuhatarisha amani katika jamii visiwani humo.

Wametoa kauli hiyo leo Jumatano Septemba 29, 2021 katika mkutano wake na viongozi hao uliofanyika Welezo Utengano Mjini Unguja.

Akisoma risala ya viongozi hao, mchungaji kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Shukuru Maloda amesema wanapata shida kubwa kupata vibali vya ujenzi wa nyumba za ibada, wakidai kuzungushwa na viongozi wa shehia bila kutoa maelekezo yoyote ili kutoa fursa kwa jamii ya Kikristo kupata huduma ya kuabudu.

“Hili linawasababisha Wakristo kukosa haki yao ya msingi ya kukusanyika pamoja na kuabudu kama ilivyo kwenye katiba ya Zanzibar ibara ya 20 (1),” amesema Mchungaji Maloda

“Ombi letu kwako, utaratibu wa kupata vibali wa ujenzi wa makanisa uangaliwe upya, tunafahamu Serikali inafuata misingi ya kidemokrasia lakini tunapenda kukumbusha kwamba demokrasia pia ni pamoja na kujali mahitaji na haki za wachache,” amesema.

Pia, wameomba watoto wa kikristo wasilazimishwe kusoma masomo ya kiislamu au lugha ya kiarabu shuleni kama ilivyo sasa ambapo ni kwenda kinyume na mtalaa wa elimu.

Kuhusu lugha, wamesema wakati mtalaa wa elimu wa Zanzibar suala hilo lipo wazi, ambapo wanafunzi wanapewa fursa ya kuchagua somo au lugha ya ziada katika Kiarabu, Kiitaliano, Kifaransa, Kijerumani au Kispaniola, lakini kwa Zanzibar wamesema hayazingatiwi.

Changamoto nyingine iliyowasilishwa kwa Dk Mwinyi ni upatikanaji wa vibali vya watumishi wa kanisa ambao sio raia wa Tanzania, licha ya kutumia muda mrefu kutolewa lakini vinatozwa gharama kubwa ilhali watumishi hao wanakuwa ni wakijitolea katika huduma za jamii.

Mchungaji Maloda amesema pia kumekuwapo na ujenzi holela wa nyumba za ibada unaosababisha kujengwa karibu nyumba ya ibada na nyumba nyingine akitolea mfano kujengwa msikiti karibu na kanisa au kanisa karibu na msikiti ambapo vinaleta mgongano na misuaguano kwa wnanchi.

Naye katibu wa baraza Timoty Philemon, amesema Wakristo wamefarijika kukutana na Dk Mwinyi huku akimuomba utarattibu huo uendelee ili wazidi kumueleza mambo mbalimbali waliyo nayo katika kanisa na kwenye jamii.