Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 20Article 547690

Habari Kuu of Tuesday, 20 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mabadiliko Sheria ya Ushirika  kuleta neema kwa wanachama

Mabadiliko Sheria ya Ushirika   kuleta neema kwa wanachama Mabadiliko Sheria ya Ushirika  kuleta neema kwa wanachama

WANACHAMA wa vyama vya ushirika nchini sasa wana kila sababu ya kufurahi baada ya serikali kusikiliza kilio chao cha miaka mingi kutaka Sheria ya Ushirika ya mwaka 2013 ifanyiwe marekebisho ili kuvipa mamlaka kamili ya kuhakikisha mali na shughuli zote za vyama hivyo zinasimamiwa na wanachama wenyewe.

Kimsingi, vyama vya ushirika ni nguzo muhimu kwa wanachama wake kwani huwapa fursa ya uwekezaji nafuu wa huduma za kifedha pamoja na ushauri madhubuti ambao huwasaidia kuboresha maisha yao kiuchumi pamoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, vyama hivi vimekuwa vikikabiliwa na matatizo yanayofanana karibu nchi nzima, ambayo husababishwa na mfumo mbovu wa kisheria, matumizi mabaya ya fedha za ushirika, uongozi mbaya na maamuzi yasiyoridhisha kutoka kwa wanasiasa.

Ndiyo maana baada ya kuliona hili, Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, ametangaza mikakati ya serikali iliyopo hivi sasa ya kuifanyia marekebishi sheria inayovisimamia vyama vya ushirika huku akisisitiza kuwa serikali inatekeleza azma hiyo kwa kushirikia na na wadau wote wa ushirika nchini.

Profesa Mkenda alitoa kauli hiyo hivi karibuni mjini Tabora wakati wa hafla ya maadhimisho ya siku ya ushirika duniani iliyofanyika kitaifa mkoani Tabora.

Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo yaliyokuwa na kaulimbiu ‘Ushirika Pamoja, Tujenge Upya kwa Ubora na Tija’ alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Waziri Mkenda alitumia jukwaa la maadhimisho hayo kueleza mikakati mbalimbali ambayo serikali inapanga katika kutekeleza mipango mbalimbali ya kuendeleza ushirika nchini.

Miongoni mwa mikakati hiyo, anasema, ni mchakato unaoendelea wa kutungwa kwa sheria mpya inayosimamia ushirika, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa na wadau wa ushirika kuwa inakwamisha utekelezaji wa shughuli zao.

Pamoja na mambo mengine, ni wazi kuwa ushirika una mchango mkubwa katika upatikanaji wa rasilimali fedha, kuyapa thamani mazao ya kilimo pamoja na utafutaji wa masoko ya bidhaa za kilimo.

Vyama vya ushirika vimechangia kiasi kikubwa katika kuinua maisha ya watu maskini, kuongeza usalama wa chakula nchini pamoja na kutengeneza fursa za ajira ambazo zimesaidia kupunguza umaskini.

Kutokana na hali hiyo, ni wazi kwamba vyama vya ushirika ni chachu katika kuhamasisha utunzaji wa akiba katika maendeleo ya watu na taifa kwa ujumla, hivyo, mabadiliko ambayo hutokea katika ushirika huleta pia mabadiliko chanya au hasi katika jamii.

Kupitia mabadiliko yanayotarajiwa kuwepo kwenye sheria, Mkenda anasisitiza kuwa yatavisaidia vyama vya ushirika kutekeleza majukumu yao bila kuingiliwa na wanasiasa au viongozi wa serikali kama ilivyo sasa.

“Kabla hatujapeleka muswada bungeni, serikali itawashirikisha wadau wote wa ushirika ili watoe maoni yao ambayo yatajumuishwa katika rasimu tunayoiandaa ili tuje na sheria bora zaidi ambayo italinda maslahi ya wanaushirika wote,’’ anasema waziri.

Anaongeza: “Sheria iliyopo hivi sasa ilitungwa mwaka 2001 na baadaye kufanyiwa marekebisho mwaka 2013 na safari hii tunatarajia kuja na sheria nzuri zaidi ambayo haitakuwa kikwazo kwenye ushirika.’’

Profesa Mkenda anasema nia ya serikali ni kuongeza uwajibikaji mkubwa zaidi wa vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa (SACCOS) na vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) nchini.

“Tunawaomba hata viongozi wastaafu wa vyama vya ushirika kuipitia rasimu ya sheria mpya ili watoe maoni yao ambayo yatatusaidia kuja na sheria mpya nzuri itakayowezesha kukuza ushirika hapa nchini,’’ anasisitiza.

Akihutubia mamia ya wanachama vya vyama vya ushirika mjini Tabora, waziri huyo wa kilimo pia anasisitiza kuwa hakuna ruhusa kwa kiongozi yeyote kwenda kuwapangia matumizi ya fedha wanaushirika.

“Ushirika ni hiari na ni mali ya wanaushirika, hivyo wanachama wanatakiwa kujua kwamba ni mali yao, wasimame kidete kusimamia shughuli zao bila kuingiliwa kinyume na utaratibu, na sisi viongozi wa serikali lazima tujue mipaka yetu,’’ anasema.

Hata hivyo, Waziri Mkenda anasema serikali bado ina wajibu kwenye ushirika kwa sababu wanaushirika ni wengi na kuna viongozi wao na pia kuna sheria inayowatambua.

“Ndani ya serikali kazi yetu ni kuhakikisha sheria inafuatwa, viongozi wanawajibika kwa wanaushirika wao na maamuzi yote ya wanaushirika yanafanywa na wanachama na si kukundi tu cha watu wachache,’’ anasema.

Anasema serikali itaendelea kusimamia ushirika ili kuhakikisha unasimamiwa kwa weledi, uwajibikaji na uwazi ili kuona watu wengi wanapenda na kukubali kujiunga na vikundi mbalimbali vya ushirika kwa ajili ya maendeleo yao.

Hivi karibuni Naibu Waziri wa kilimo, Hussein Bashe alilieleza Bunge kuwa serikali inafahamu changamoto zinazovikabili vyama vya ushirika na kwamba inaendelea kuzitafutia ufumbuzi, ikiwemo mchakato unaoendelea wa kutungwa kwa sheria mpya inayovisimamia vyama hivyo.

“Sheria itakayotungwa itazingatia matakwa ya sasa ambayo pia yataangalia mabadiliko katika mifumo ya uongozi wa ushirika ili kwenda na teknolojia ya kisasa itakayoviwezesha vyama vya ushirika kuimili ushindani,” alisema.

Bashe alisema serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha rasimu ya sheria hiyo ambayo itashughulikia changamoto zote zinazoukabili ushirika ambazo zinachangiwa na upungufu wa sheria iliyopo hivi sasa.

Katika siku hiyo ya maadhimisho ya siku ya ushirika duniani ambayo huadhimishwa kila Jumamosi ya kwanza ya mwezi Julai, Profesa Mkenda alidokeza kuwa serikali imeshatoa mikopo katika vyama vya ushirika inayofikia kiasi cha shilingi trilioni 1.5 kwa ajili ya kukuza ushirika hapa nchini.

Madhumuni ya maadhimisho haya ni kuongeza uelewa kwa wanaushirika na kuimarisha mafanikio ya umoja wa kimataifa, uchumi endelevu, usawa na amani kote duniani.

Siku hii pia ina lengo la kuendeleza na kutanua ushirikiano baina ya ushirika wa kimataifa na nchi zingine duniani ikiwemo kushirikisha serikali kwa ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Mbali na kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 1.5, Prof Mkenda anasema kupitia ushirika bei ya pamba imepanda.

“Aliyesababisha bei ya pamba kupanda ni chama cha ushirika cha Kahama (KACU) na mwaka huu tutakuwa na bei nzuri ya pamba na haya ni mafanikio makubwa sana katika vyama vya ushirika,” anasema Waziri.

Anasema serikali bado ina matumaini makubwa kwenye ushirika na kwamba itaendelea kusimamia ushirika nchini ili kuhakikisha unaendelea kukua na kuinua maisha ya wakulima, wafugaji, wavuvi na watanzania wote kwa ujumla.

Katika kuhakikisha kuwa serikali inaimarisha ushirika nchini, serikali katika bajeti ya Wizara ya Kilimo katika mwaka wa fedha wa 2021/22 imesisitiza kuwa itaendelea kuiwezesha Tume ya Maendelea ya Ushirika Tanzania (TCDC) ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Kilimo Mei 4 mwaka huu, Prof Mkenda alisema kuwa katika mwaka huu wa fedha, TCDC itaendelea na programu zake za mafunzo kwa ushirika kote nchini hususan katika masuala ya uagizaji bidhaa kwa pamoja ili kuepuka gharama zisizo na tija.

Alisema kuwa mafunzo pia yatajikita katika kuhakikisha kwamba maslahi ya ushirika nchini yanasimamiwa ili kunufaisha wanachama walio wengi badala ya vikundi vichache vya watu binafsi.

“Hili litaenda sambamba na ukaguzi wa jumla wa mali za vyama vya ushirika pamoja na kufanya ukaguzi wa nje katika vyama vipatavyo 6,500 nchi nzima,’’ alisisitiza.