Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 14Article 551473

Habari za Mikoani of Saturday, 14 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mabasi mapya 70 mwendo kasi yaanza huduma Dar

Mabasi ya Mwendokasi Mabasi ya Mwendokasi

HUDUMA katika usafiri wa mabasi yaendayo haraka mkoani Dar es Salaam zinaendelea kuboreshwa baada ya mabasi mengine 70 mapya kuingizwa barabarani na kufanya kuwa na jumla ya mabasi 210.

Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Philemon Mzee, alisema Dar es Salaam jana kuwa, utaratibu wa manunuzi wa mabasi mengine ili kukidhi mabasi 305 yanayohitajika katika mradi huo awamu ya kwanza, unaendelea.

Akizungumza katika hafla ya kuanza safari kwa mabasi hayo mapya yanayotoa huduma kati ya Kimara hadi Kivukoni na Gerezani, Mzee alisema hatua ya kuingia barabarani kwa mabasi hayo itaboresha huduma za usafiri mkoani Dar es Salaam.

Alisema mabasi hayo yataanza kutoa huduma kwa njia zinazoingia njia kuu ambazo bado daladala zinatoa huduma.

Alizitaja njia hizo ambazo zitaanza huduma za mabasi ya haraka kwa awamu kuwa ni Shekilango hadi Mwenge, Morocco hadi Kawe, Morocco hadi Masaki, Shekilango hadi Magomeni Kanisani na Mwanamboka hadi Makumbusho.

“Njia hizi zinazoingia njia kuu zitafanya kazi kwa awamu baada

ya daladala kuondoka, ujenzi wake uko katika hatua mbalimbali hivyo kila njia itakapokamilika huduma zitaanza kutolewa kwa kutumia mabasi hayo 210 yaliyopo sasa,” alisema.

Amesema mabasi hayo ni yale 70 yenye thamani ya Dola za Marekani 270,000 yaliyokuwa yakishikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa miaka kadhaa kwa kushindwa kulipia kodi ili kuyatoa bandarini.

Mzee alisema magari hayo yatasaidia kuongeza wigo wa uendeshaji ikiwa ni pamoja na kumsimamia mtoa huduma kuhakikisha anafuata utaratibu wa kusimamia mabasi hayo na kufanyia ukarabati inapohitajika ili kuepuka kuharibika.

“Kwa sasa tunaendelea na utaratibu wa kuhakikisha mabasi yote yanafanya kazi ikiwemo yale yaliyokuwa mabovu yaliyokuwa yamesimama bila kutoa huduma,” alisema Mzee.

Alibainisha kuwa ujenzi wa awamu ya pili ya mradi huo kutoka Kariakoo hadi Mbagala unaendelea na utakamilika Machi, 2023 katika ujenzi wa barabara huku ujenzi wa vituo ukikamilika mwisho wa mwezi huu.

Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara katika mradi huo na kujionea mabasi kadhaa yakiwa yameharibika na kutelekezwa na kusababisha kumfuta kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha wa DART, Suzan Chaula kwa kutoridhishwa na utendaji kazi wake .