Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 17Article 552013

Habari za Mikoani of Tuesday, 17 August 2021

Chanzo: eatv.tv

Mabasi yatajwa kuchangia ongezeko Watoto Mitaani

Mabasi yatajwa kuchangia ongezeko Watoto Mitaani Mabasi yatajwa kuchangia ongezeko Watoto Mitaani

Baadhi ya wamiliki wa mabasi wametajwa kuchangia ongezeko la watoto waoishi na kufanya kazi mitaani kutokana na kusafiri na Watoto bila kuwa na Watu wazima wala kufahamu wanaelekea huko kufanya nini.

Hali hiyo imebainika wakati Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu alipotembelea vituo vya kuhudumia watoto hao ambao wamemueleza wanavyosafiri kutoka Mikoani kwenda jijini Dar es Salaam kwa nauli pungufu.

Dkt. Jingu pia ametoa wito kwa mashirika mengine yote yanayofanya kazi ya kuwasaidia watoto hao kuhakikisha wanawarekebisha na kuwarudisha nyumbani kwao mapema.

"Lazima tuongee na LATRA ili tuweze kukaa na wenye mabasi ili kuliweka sawa suala hili, haiwezekani mtoto mdogo hana mtu anayeambatana naye unampakia, ni jukumu letu wote kuwalinda bila kujali ni wako au siyo wako" amesema Dkt. Jingu.Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiwasikiliza Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika Kituo cha Babawatoto kilichopo Mburahati, Wilaya ya Ubungo, mkoa wa Dar es salaam.

Awali akiwasilisha taarifa ya utoaji wa huduma za shirika hilo, Meneja mradi wa kituo Johnson Mtango amesema kutokana na jitihada wanazofanya za kuwatoa watoto mitaani na kuwapatia huduma, inaonesha tatizo kupungua kwani utafiti uliofanywa mwaka 2017 na 2021 kulikuwa na watoto 2,504 mitaani lakini sasa hivi watoto ni 1,504 kwa mkoa wa Dar es salaam pekee.

Amesema hata hivyo changamoto bado ipo kwani kuna ongezeko la watoto wapya kila siku kuingia mjini wakitokea mikoani na kupitia vituo vya mabasi hususani Kituo kikuu cha Mbezi na  Mbagala Rangi Tatu.

"Sababu za watoto kukimbilia mijini ni kukosa malezi bora, umasikini na ushawishi wa wenzao, inaonesha tatizo limepungua lakini bado Kuna changamoto ya watoto wapya kuja mitaani." aliongeza Mtango.