Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 29Article 560428

Habari za Mikoani of Wednesday, 29 September 2021

Chanzo: Mwananchi

Madereva wailalamikia Latra kubadilisha ratiba za safari

Madereva wailalamikia Latra kubadilisha ratiba za safari Madereva wailalamikia Latra kubadilisha ratiba za safari

Madereva wa mabasi yanayofanya safari za Dar es Salaam- Mbeya wameilalamikia Mamlaka ya Udhibiti usafiri Ardhini (Latra) kubadili ratiba ya safari, hivyo kuwalazimu kupaki mabasi porini ili kusubiri muda wa kuvuka kituo cha ukaguzi cha Mbeya.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano Septemba 29, 2021, baadhi ya madereva wamesema kuwa ratiba hiyo imebadilishwa kwa njia ya Mikoa ya Mbeya na Iringa na wao hawakushirikishwa.

"Unakuta Dar es Salaam unatoka saa 12 asubuhi na ratiba inaonyesha tunapaswa kufika katika kituo cha ukaguzi kati ya Mkoa wa Iringa na Mbeya majira ya saa 11.45 jioni ambapo awali walikuwa wakifika 10.45 za jioni hivyo ukiangalia ratiba hiyo imekuwa ngumu na kandamizi kwetu madereva na kero kwa abiria," amesema mmoja wa madereva ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Dereva wa basi la kampuni ya Newforce, Juma Abdul amesema kuwa hiyo ni changamoto kubwa, kwani maeneo ambayo wanasimama sio rafiki na yanahatarisha usalama wa abiria na mali zao, akimwomba Waziri mwenye dhamana kuingilia kati suala hilo.

Dereva wa Kampuni ya mabasi ya Sauli, Matokeo Langasi amesema kuwa mabadiliko ya ratiba za masafa mara kwa mara ni changamoto kwao, kwani huathiri biashara ya usafirishaji.

Naye abiria aliyekuwa akisafiri kutoka jijini Dar es Salaam kuja mkoani Mbeya, Sakina Joshua amesema maporini wanakosimamishwa hakuna usalama wala huduma ya vyoo, maji na chakula.

Mwanasheria wa Madereva Tanzania, Frank Bonerge, amesema kuwa amepata malalamiko na kuomba Serikali iyashughulikie.

"Nimelazimika kuja mkoani Mbeya katika mpaka wa Iringa na Mbeya kutokana na kuwepo kwa malalamiko ya madereva kubadilishiwa ratiba ya masafa na Latra na ni kweli nimejionea hali hiyo," amesema Bonerge.

Meneja wa Latra Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Denis Daudi amekiri mamlaka hiyo kubadili ratiba akisema mabadiliko hayo yalifanywa kwa makubaliano kwenye kikao cha wadau wa usafiri kwa lengo la kuwezesha kupunguza ajali za barabarani.