Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 26Article 539932

Habari Kuu of Wednesday, 26 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Maghala 14 kudhibiti sumukuvu Bara, Z’bar

Maghala 14 kudhibiti sumukuvu Bara, Z’bar Maghala 14 kudhibiti sumukuvu Bara, Z’bar

WIZARA ya Kilimo inajenga maghala 14 yakiwamo mawili visiwani Zanzibar kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Udhibiti wa Sumukuvu Tanzania (Tanipac).

Waziri wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda alisema jana kuwa, mradi huo unatekelezwa kwa lengo la kudhibiti sumukuvu nchini ili kupunguza athari katika mazao ya chakula hasa karanga na mahindi.

Aliyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Alisema lengo la mradi huo utakaokuwa na maghala 12 Tanzania Bara utaimarisha usalama wa chakula, kulinda afya ya mlaji na kuongeza biashara ya nje.

Alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa kituo cha taifa cha kibaiolojia (Kibaha), kituo mahiri cha usimamizi wa mazao ya nafaka baada ya kuvuna (Mtanana, Kibaigwa) na maabara kuu ya kilimo (Dodoma).

Profesa Mkenda alisema maghala hayo 14 yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 34,000 za nafaka katika wilaya za Chemba, Kiteto, Babati, Gairo, Namtumbo, Namyumbu, Itilima, Kasulu, Kibondo, Buchosa, Bukombe na Kilosa na Zanzibar.

Tanipac pia itawapatia vifaa vijana 400 katika mikoa ya Dodoma, Mwanza, Manyara, Kigoma, Tabora, Ruvuma, Mtwara, Morogoro na Geita kwa ajili ya kutengeneza vihenge vya chuma visivyoruhusu hewa vya kuhifadhi nafaka katika ngazi ya kaya.

Waziri huyo alisema pia Tanipac imetoa mafunzo ya kilimo bora yanayolenga kudhibiti sumukuvu kwenye mazao ya mahindi na karanga.

Pia alisema mradi huo umetoa mafunzo kwa maofisa ugani 261 katika wilaya za Kiteto (58), Babati (60), Kilosa (105) na Gairo (38).

Profesa Mkenda alisema katika mafunzo hayo wajumbe wote wa timu ya uongozi (CMT) katika halmashauri hizo walielimishwa kuhusu sumukuvu na kuelekezwa kazi zitakazofanyika na majukumu yao ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.

Aidha, waandishi wa habari 30 wa vyombo vya habari vya Zanzibar wamepatiwa mafunzo maalumu kuhusu namna bora ya kuhabarisha umma juu ya sumukuvu na madhara yake kwa afya ya binadamu na biashara ya nje.

Alisema mafunzo kama hayo yatafanyika Tanzania Bara kwa waandishi wa habari zaidi ya 105.

Join our Newsletter