Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 21Article 573106

Uhalifu & Adhabu of Sunday, 21 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mahakama yamtia hatiani Mhandisi wa Maji kwa rushwa

Mahakama yamtia hatiani Mhandisi wa Maji kwa rushwa Mahakama yamtia hatiani Mhandisi wa Maji kwa rushwa

Mahakama ya Wilaya ya Geita imemhukumu Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Rahel Anthony kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini kwa makosa mawili ya rushwa.

Hukumu hiyo ya kifungo au kulipa faini ya Sh milioni kwa kila kosa, ilitolewa baada ya kukutwa na hatia ya kosa la kujipatia Sh milioni 75 kinyume cha sheria.

Akisoma hukumu hiyo Novemba 16 mwaka huu, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Geita, Samuel Maweda alisema mshitakiwa alitenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 16(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007.

Maweda alieleza kuwa mshitakiwa alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Oktoba 30, mwaka 2019 na alisomewa na kukana mashitaka hivyo kulazimu upande wa mashitaka kuleta ushahidi kwa lengo la kuthibitisha makosa. Awali, Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo, Kelvin Murusuri aliieleza mahakama kwamba katika Machi 11, 2019 mshitakiwa alijipatia Sh milioni 25 na mara nyingine Sh milioni 50 kutoka kwa Mkurugenzi wa Fare Tanzania Ltd, Francis Nyenge.

Alisema mshitakiwa alifanya hivyo kwa ajili ya kuongeza muda wa mkataba wa kusambaza mabomba ya maji kazi ambayo kampuni hiyo ilikuwa imeingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Geita katika mradi wa maji wa Chankorongo.

Mshitakiwa baada ya kutiwa hatiani, kupitia kwa wakili wake, Beatus John aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ana familia inayomtegemea. Upande wa mashitaka kupitia kwa Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Antidius Rutayuga uliomba adhabu kali kwa mshitakiwa iwe fundisho kwa watumishi wa umma wenye tabia kama hiyo.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Leonidas Felix alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa wanapohisi au kuona vinatendeka katika miradi ya maendeleo na idara za serikali na binafsi wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria