Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 15Article 551566

Habari Kuu of Sunday, 15 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Majaliwa: Mitambo iliyokwama bandarini itoke

Majaliwa: Mitambo iliyokwama bandarini itoke Majaliwa: Mitambo iliyokwama bandarini itoke

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameagiza mawaziri wa wizara mbili pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, kukutana kukamilisha taratibu za utoaji wa mitambo ya ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Mbigiri iliyokwama bandarini.

Mawaziri walioagizwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda.

Alitoa maagizo hayo jana baada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho, alipotembelea mradi wa shamba la miwa la Mkulazi pamoja na kukagua ujenzi wa kiwanda cha sukari Mbigiri, mkoani Morogoro.

Katika taarifa hiyo Waziri Mkuu alielezwa kuwa kuna baadhi ya mitambo ya ujenzi wa kiwanda imekwama bandarini.

“Tunataka kiwanda hiki kianze kujengwa, ucheleweshwaji usio na umuhimu hatuupi nafasi, hatutaki ujenzi ukwame, zile kontena 21 kule bandarini tunataka zitoke Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha na Mipango na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu mkae mkokotoe kile kinachopaswa kulipwa kijulikane mitambo ile itoke,” alisema.

Alisema kwa namna nchi ilivyojipanga katika ujenzi wa viwanda, Tanzania itakuwa na viwanda saba vya sukari lengo likiwa ni kuhakikisha inajitosheleza kwa kuwa na sukari ya kutosha na kuondoa pengo la tani 70,000 lililopo, hivyo kupunguza uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.

Wakati huo huo Majaliwa aliipongeza Bodi ya Mkulazi, watendaji wa shamba la Miwa la Mkulazi pamoja na uongozi wa kiwanda cha Sukari cha Mbigiri kwa usimamizi mzuri wa mradi huo kutokana na hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa.

“Kwetu sisi Watanzania mradi huu ni muhimu sana, nilikuja hapa mwaka 2018 sikukuta hali hii ninayoiona leo, miwa ilikuwa inaonekana kando kando ya barabara

tu lakini leo nimekuta mabadiliko makubwa miwa inaonekana katika shamba lote na nimekuta harakati za ujenzi wa kiwanda cha sukari ambacho kipo katika hatua ya msingi, hongereni sana.”

Kutokana na kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho cha Sukari cha Mbigiri, Waziri Mkuu aliwasihi wananchi wanaoishi pembezoni mwa eneo hilo walime miwa kwa wingi kwa kuwa wana soko la uhakika la kuuza zao hilo.

Aliagiza pia uongozi wa Wilaya ya Kilosa uhakikishe kila mwananchi anayetaka kulima miwa anapata ardhi kulingana na mahitaji yake.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha mazingira ya ukuaji wa uchumi nchini hususani kwa mwananchi mmoja mmoja. Aliwasisitiza wananchi kuchangamkia fursa za maendeleo zilizopo katika maeneo yao zikiwemo za kilimo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Medard Kalemani amempa siku saba Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wa Wilaya ya Kilosa awe amepelekea umeme katika visima vya wakulima wa miwa ambao kwa sasa wanatumia jenereta kuzalisha umeme.

Meneja wa shamba la Miwa la Mkulazi, Flavian Regonard, alisema wameshaanza kuvuna miwa katika shamba hilo na wanaiuza katika kiwanda cha Sukari cha Mtibwa kwa kuwa hawajaanza uzalishaji wa sukari.

Eneo lililopandwa miwa kwa sasa ni hekta 2,705 na kwa mwaka huu wanatarajia kuendeleza shamba kwa kupanda hekta 800.