Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 19Article 543376

Habari Kuu of Saturday, 19 June 2021

Chanzo: eatv.tv

Majaliwa aagiza wafanyakazi wawili EPZA kuondolewa

Majaliwa aagiza wafanyakazi wawili EPZA kuondolewa Majaliwa aagiza wafanyakazi wawili EPZA kuondolewa

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda Dotto James kuwaondoa watumishi wawili wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) wilayani Ubungo ambao ni Sara Mwaipopo na Grace Lemunge kwa sababu ya ufanyaji kazi wa mazoea na urasimu.

Waziri Mkuu Majaliwa amaetoa agizo hilo katika ziara yake katika mamlaka hiyo ambapo amesema hajaridhishwa na viwango vya uwekezaji kwa sababu ya urasimu uliokuwepo EPZA na amewataka watumishi wabadilike.

"Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda Dotto James waondoe hapa Mkuu wa Kitengo cha Sheria Sara Mwaipopo na Meneja Uwezeshaji Grace Lemunge kwa sababu wanafanyakazi kwa mazoea na urasimu mkubwa. Hapa hatuhitaji urasimu, tunataka wawekezaji," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa ameagiza kutafutwa watu wote waliohusika na ung’oaji wa vifaa ikiwemo jenereta katika moja ya jengo hilo.

“Hatua kali zichukuliwe kwa aliyeng’oa vitu katika jengo lile, lazima kazi ifanyike kwa kuzingatia weledi, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona kazi zikiwa zimeshamiri hapa na eneo hili livutie wawekezaji, tunataka mambo yaende vizuri ili nchi izidi kupata maendeleo,” amesema Mhe. Majaliwa.    “Hivi jenereta hapa linaibiwaje na linapitaje katika geti?, si rahisi mtu atoke Mbagala aje aibe hapa mmeiba nyie wenyewe, Mkurugenzi fuatilia kujua nani anaiba vifaa kwa sababu hakuna mtu anayeweza kuingia katika eneo hili bila ya kufuata taratibu,” ameongeza Mhe. Majaliwa.   Waziri Mkuu alitembelea maeneo mengine pamoja na kiwanda cha kushona suruali za jeans cha Tooku ambacho soko kubwa la bidhaa zake lipo nchini Marekani na kiwanda cha nafaka cha Somani.