Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 28Article 566302

Habari Kuu of Thursday, 28 October 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Majaliwa afichua maajabu sita ya Rais Samia

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametaja vipaumbele sita vya kiutekelezaji vilivyofanywa na Rais Samia katika kipindi cha miezi sita tangu aingie madarakani na kusema kuwa tayari ameonesha dira na nia thabiti katika kuwaletea maendeleo Watanzania.

Waziri Mkuu amesema katika kipindi kifupi Rais Samia ametoa fedha nyingi ambazo zimekwenda moja kwa moja katika kutekeleza miradi hiyo ikiwemo afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara, nishati na rasilimali watu.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua na kushiriki ujenzi wa kituo kipya cha afya kinachojengwa katikati ya Vijiji vya Mvuleni na Kijiweni kwenye jimbo la Mchinga Mkoani Lindi.

Ameongeza kusema kuwa katika sekta ya elimu Rais Samia amewezesha ujenzi wa madarasa katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na shule mpya ikiwa ni sehemu ya mkakati mahususi wa kuhakikisha watoto wanapata elimu bora kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari na tayari fedha zimetolewa kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Kwa upande wa Nishati, amesema Rais Samia ameendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi ya uzalishaji wa nishati ya uhakika ikienda sambamba na kuunganisha mikoa yote na umeme wa gridi ya Taifa kazi ambayo inaendelea nchini kote.

Amesisitiza kuwa miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ni muendelezo wa mkakati madhubuti wa Rais Samia wa kumtua mama ndoo kichwani kampeni ambayo utekelezaji wake umeanza kuzaa matunda ambapo hivi karibuni Rais alizindua mradi wa maji wa Longido Mkoani Arusha.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha sekta ya rasilimali watu na ajira kwa kufanya maboresho ya maslahi ya watumishi na tayari kada mbalimbali za watumishi wa umma wamepandishwa vyeo na madaraja ikiendana sambamba na malipo ya malimbikizo ya madeni.