Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 23Article 573640

Habari Kuu of Tuesday, 23 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Majaliwa ahimiza sensa ya watu na makazi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka watu kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi inalotarajiwa kufanyika mwaka 2022 ili kuiwezesha Serikali kupanga maendeleo, kupunguza umasikini na kukuza uchumi.

Majaliwa ametoa rai hiyo wakati akizindua Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kilichoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

“Matokeo ya sensa yataiwezesha Serikali kupata takwimu za msingi zinazotumika kuakisi hali halisi iliyopo na kupanga mipango ya maendeleo kwa kutunga sera pamoja na kupanga mipango, program na kufuatilia utekelezaji wake”, amesema Majaliwa katika taarifa iliyotumwa na kitengo cha mawasiliano Serikalini cha wizara hiyo.

Amesema ni muhimu wananchi watoe ushirikiano kwa wakusanya takwimu ili kuliwezesha zoezi hilo kuenda vizuri na kuleta matokeo tarajiwa kwa maendeleo ya nchi.

Aidha, amewataka wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuanza kutoa elimu ya umuhimu wa sensa kwa wananchi ili kuwaweka tayari kushiriki zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah amesema anaamini kuwa sensa ya mwaka 2022 itakuwa ya kipekee kutokana na juhudi za viongozi na wataalamu waliopo ambao wamesha ainisha changamoto zote zilizojitokeza katika sensa zilizopita na kupanga namna bora ya kuzitatua kwa ajili ya kuboresha.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Yussuf Masauni amesema Serikali inawajibu wa kuandaa zoezi la sensa ya watu na makazi ili kupata idadi kamili ya watu na kuweza kupanga maendeleo ili kukuza uchumi.

Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema kuwa uzinduzi wa kitabu cha Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ni alama kuu ya uzinduzi rasmi wa shughuli za maandalizi ya sensa hiyo ambayo majaribio yake yatafanyika Agosti, 2021.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa amesema sensa hiyo itakuwa ya kipekee kwa kuwa itatumia teknolojia ya hali ya juu ili kupata taarifa kuanzia kwenye ngazi ya vitongoji, vijiji na ngazi ya mitaa na mijini.