Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 30Article 544804

Habari Kuu of Wednesday, 30 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Majaliwa aonya mafisadi mpango wa maendeleo

Majaliwa aonya mafisadi mpango wa maendeleo Majaliwa aonya mafisadi mpango wa maendeleo

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kutekeleza malengo ya Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo na haitafumbia macho ukwepaji kodi, uzembe kazini, ufujaji wa fedha na rushwa.

Majaliwa amesema hayo jijini Dodoma wakati akizindua mpango huo wa miaka mitano (2021/22- 2025/26) kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele vitano utakaoghamu Sh trilioni 114.8.

Aliagiza wizara, taasisi za umma, wakala wa serikali, idara zinazojitegemea, wadau wa maendeleo na sekta binafsi na wananchi kwa ujumla wahakikishe wana nakala za mpango huo ili kutekeleza kwa pamoja.

“Serikali imedhamiria kutekeleza mpango huo, fedha za kutekeleza zikipatikana, utatekelezwa kwa zaidi ya asilimia 100 kwa sababu ni shirikishi sekta mbalimbali zikiwemo taasisi na mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, watu binafsi,” alisema Majaliwa na kuongeza kuwa katika fedha hizo za kutekeleza mpango huo, Sh trilioni 74.2 zitatoka serikalini na sekta binafsi itachangia Sh trilioni 40.6. Sh trilioni 107 zilitumika kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo hivyo ni ongezeko la asilimia 6.7, lakini pia mchango wa serikali katika kutekeleza mpango wa sasa umeongezeka kwa asilimia 17.8.

Majaliwa alisema mpango wa tatu una vipaumbele vitano kikiwemo cha kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani, kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuendeleza rasilimali watu, kuchochea maendeleo ya watu na kukuza uwekezaji na biashara.

Mpango huo pia utaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo na programu zinazofungua fursa za kiuchumi, ujenzi wa uchumi wa viwanda, kuongeza ushindani wa bidhaa nchini katika masoko ya kikanda na kimataifa pamoja na maendeleo ya watu.

Utekelezaji wa mpango huo utawezesha kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa, Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) wa megawati 2,115, kuboresha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Tanga, Tanzania.

Pia utaendeleza Kiwanda cha Sukari-Mkulazi, ujenzi wa madaraja makubwa na madaraja ya juu, kufua umeme wa maji wa Ruhuji wa megawati 358 na kutekeleza Mradi wa Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na chuma Liganga.

Utekelezaji huo pia utawezesha ununuzi wa meli za uvuvi na ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Mbegani, kufua umeme wa maji wa Rumakali wa megawati 222, utafutaji wa mafuta na gesi katika Kitalu cha Eyasi Wembere.

Mpango huo pia utawezesha usindikaji gesi asilia (LNG) Lindi na ujenzi wa reli ya kusini, kuendeleza kanda maalumu za kiuchumi na maeneo maalumu ya uwekezaji na mradi wa magari soda wa Enguruka.

Pia kufanya ufuatiliaji wa mafuta na gesi wa Mnazi Bay Kaskazini pamoja na kuongeza raslimali watu wenye ujuzi adimu na maalumu kwa maendeleo ya viwanda na ustawi wa jamii nchini.

Mpango huo unakusudia kujenga viwanda, kuchochea viwanda na kuimarisha wa uzalishaii wa ndani na utoaji huduma. Kukuweza uwekezaji na biashara na kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza raslimali.

Mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Ilani ya CCM 2020, Mpango wa Maendeleo elekezi wa 2011/12-25/26, matokeo ya tathmini huru iliyofanywa kuhusu mpango wa pili, sera na mikakati ya kisekta.

Pia kwa kuzingatia matokeo ya utafiti na vyuo na taasisi, Dira ya Afrika Mashariki (EAC) 2050, Dira ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 2050, Ajenda ya Maendeleo ya Afrika ya 2063, Mpango wa Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs) ya 2030 na Makubaliano ya Kimataifa ya Paris ya Mabadiliko ya Tabianchi.

Majaliwa alisema mpango wa pili unakamilishwa leo Juni 30, 2021 na umepata mafanikio makubwa kutokana na tathmini iliyofanywa na mtathimini huru.

“Miongoni mwa mafanikio hayo taifa kuingia katika kundi la uchumi wa kati Julai 2020, kipato cha wastani cha kila mtu kuongezeka 2,225,099 sawa na dola 1022 katika mwaka 2016 hadi mwaka 2020, 2,653,790 sawa na dola 1,151 ni kielelezo cha tosha cha mafanikio makubwa kuelekea maendeleo makubwa,” alisema Majaliwa.

Mafanikio hayo yalichangiwa na jitihada za kila mmoja kufanya kazi kwa bidii na uaminifu, uthubutu wa serikali kutekeleza yale yote yaliyoahidiwa, sera nzuri za fedha, ki bajeti na kufungamanisha ukuaji uchumi na maendeleo ya watu chachu kupungua kuwa sababu kuondoa umaskini.

Sekta zilizochangia kupata mafanikio hayo ni pamoja na elimu, umeme, afya, kilimo, viwanda, usafirishaji, kuondoa umaskini na biashara za mipakani.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Yusufu Masauni alisema mpango wa tatu ni shirikishi, umeshirikisha wadau kuanzia kwenye maandalizi hadi uzinduzi wake hivyo hata utaekelezaji utakuwa na mafanikio.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema Mpango wa Tatu wa Maendeleo umeandaliwa sanjari na utekelezaji wa mikakati yake ya utekelezaji ukiwemo mpango kazi wa utekelezaji mpango, mkakati wa ugharimishaji wa mpango, mkakati wa utuatiliaji na tahtmini ya utekelezaji mpango.