Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 10Article 584584

Habari Kuu of Monday, 10 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Majaliwa ataka kasi miradi ya ujenzi Z’bar

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi na watendaji wanaosimamia miradi ya ujenzi waongeze kasi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuwapa fursa wananchi wafaidi matunda ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar.

Ametoa wito huo jana wakati akizungumza na wakazi wa Jimbo la Kiwani, Mkoa wa Kusini Pemba mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha afya cha shehia ya Kendwa ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za sherehe ya miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar.

“Niwaombe viongozi na watendaji wanaosimamia mradi huu waendelee kushirikiana na kufanya kazi kwa kasi zaidi ili kukamilisha ujenzi huu kwa wakati uliopangwa ili kuwapa fursa wananchi wafaidi matunda ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar,”alisema.

Pia amewataka viongozi wa shehia hiyo washirikiane na Wizara ya Afya kuhakikisha majengo na miundombinu iliyowekwa inatunzwa vema ikiwemo vifaa vitakavyonunuliwa sasa kwa matumizi ya sasa na baadaye.

Akizungumzia uboreshaji wa huduma za afya, Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kujenga vituo vingi zaidi ili wananchi wasiende umbali mrefu kutafuta huduma hizo. Waziri Mkuu ambaye kabla ya kuweka jiwe la msingi alikagua majengo matatu ya kituo hicho, alisema ameridhishwa na ujenzi wake na hasa kiwango cha ubora kilichopo.

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho, Msimamizi Mkuu wa Majengo kutoka ZBA, Said Malik Said alisema ujenzi wa kituo hicho unaofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ulianza Agosti 28, mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Februari 27, mwaka huu.

“Gharama za ujenzi ni shilingi milioni 388 lakini hadi sasa zimetumika shilingi milioni 270.

Kitakapokamilika, kituo kitakuwa na majengo ya wagonjwa wa nje( OPD), maabara, chumba cha daktari, vyoo, chumba cha kumfanyia mgonjwa uchunguzi wa awali, chumba cha sindano na kufunga vidonda, kitengo cha meno, wodi ya akinamama wajawazito na nyumba ya daktari yenye uwezo wa kuchukua watumishi wawili kwa pamoja,”alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga alisema kutokana na mabadiliko ya sheria, ujenzi wa kituo kama hicho utaendelea kwenye shehia zote.

Alisema kutokana na uhakiki wa walengwa wote uliofanyika Julai 2020 hadi Januari 2021, kaya 1,992 zilisema zinaishukuru serikali na kwa hiyari yao, zikaamua kujitoa rasmi kwenye mpango wa Tasaf wa kuhudumia kaya maskini.

“Kupitia uhakiki huo, kaya nyingine 211,800 zimekiri kuondokana na hali duni, wako tayari kujitoa kwenye mpango huo baada ya miezi sita. Kutokana na uimarishaji lishe, afya na elimu, uandikishaji shuleni umeongezeka na mahudhurio pia yameongezeka,”alisema.

Alisema watoto wengi waliosaidiwa na mpango huo, walipata matokeo mazuri ya ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu. “Matokeo yake, watoto 782 waliohitimu mwaka jana, wamechaguliwa kwenda vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini. Na hawa wamesaidiwa kupata ufadhili wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu,” alisema.

Akielezea mafanikio mengine ya mradi huo, Mwamanga alisema waliwahimiza walengwa wa mradi huo kote nchini wawe wanatunza akiba kutokana na miradi wanayojishughulisha nayo.

“Matokeo yake, vikundi 23,000 kutoka maeneo 71, vyenye wanachama zaidi ya 350,000 vimeweza kujiwekea akiba ya shilingi bilioni 6.9 ambapo miongoni mwao, vimeweza kukopeshana shilingi bilioni 2.6 ili waweze kushiriki shughuli za kiuchumi,”alisema.