Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 10Article 542041

Habari Kuu of Thursday, 10 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Majaliwa atoa maagizo 9 elimu watu wazima

Majaliwa atoa maagizo 9 elimu watu wazima Majaliwa atoa maagizo 9 elimu watu wazima

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maagizo tisa kwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania (TET) ili kuimarisha utoaji huduma kwa walengwa.

Majaliwa alitoa maagizo hayo katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) wakati akifungua kongamano la siku tatu la maadhimisho ya miaka 50 ya utolewaji wa elimu ya watu wazima nchini.

Alisema kutokana na umuhimu wa TET katika ukuaji uchumi wa nchi taasisi hiyo inapaswa kujitathmini na kuwa na mwelekeo unaoendana na mahitaji ya soko.

Majaliwa aliagiza TET ipanue wigo wa utendaji kazi kufikia ngazi za wilaya kwa kwa kuwa kuna watu wenye uhitaji wa huduma hiyo ya elimu hiyo.

Pia aliitaka TET ihakikishe maofisa elimu wanaoratibu elimu ya watu wazima wanafika kila kona ya nchi kufuatilia uhitaji wa elimu inayohitajika katika eneo husika, kisha kubuni mafunzo yanayoendana na mahitaji.

Majaliwa pia aliagiza TET isimamie misingi ya uanzishwaji wake kwa kufanya kazi kulingana na miongozo.

“Lengo la kuanzishwa kwa Taasisi hii ilikuwa ni kuhakikisha Watanzania wanajua kusoma, kuhesabu na kuandika ikiwa ni njia ya awali kabisa ya kuwawezesha kuchangia kusukuma gurudumu la maendeleo”alisema,

Majaliwa aliwaagiza wakuu wa wilaya na mikoa na maofisa elimu wasimamie utekelezaji wa sera za elimu kwa watu wazima zinazotekelezwa na TET na wazichukulie kwa uzito shughuli za taasisi hiyo.

Pia aliitaka TET ibuni mafunzo yanayotoa majibu haraka kwa watu wanaoenda kusoma mafunzo ya muda mfupi ya taaluma zikiwemo za kilimo, biashara, uvuvi na mengineo.

Majaliwa alisema kutokana na kuongezeka kwa wenye uhitaji wa ujuzi walio wengi si wanaotaka kufundishwa kusoma, kuhesabu na kuandika ila pia wapo watu wazima wanahitaji kupatiwa elimu ya ujuzi katika fani mbalimbali.

”Kama mkiwa mnatoa

mafunzo ya muda mfupi mfupi ya kitaaluma kwa maana ya kozi fupi fupi itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwapatia majibu ya kero za kitaaluma ambazo zinawakabili watu wazima ambao wamekosa elimu ya ujuzi wa fani mbalimbali, hilo nalo ni jukumu ninalowaagiza mkalifanyie kazi”

Majaliwa aliagiza kuimarishwa madarasa ya mpango wa elimu kwa walioikosa (Memkwa) ambayo yanatakiwa kutumiwa pia na watu wazima waliokosa elimu ili waipate kwa urahisi.

Pia aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iandae kanzi data inayoonesha idadi ya wahitimu kutoka TET kila mwaka sanjari na kuonesha ujuzi walioupata ili kuisaidia serikali kufahamu uwezo wa chuo hicho kuhudumia Watanzania.

Alisema watu wazima waliosoma kupitia TET wamekuwa msaada kwa maendeleo ya nchi hasa kwa kufanya kazi za kimaendeleo katika maeneo wanaoishi.

Pia aliwataka watafiti kutoka TET kwa kushirikiana na wenzao wa UDSM wafanye tafiti ili kubainisha namna bora ya kutoa mafunzo.

“Najua kuna mafunzo mnatoa kwa wanaotaka kusoma hadi kidato cha nne au sita kulingana na urahisi mliouweka kwenye mafunzo yenu, ila kuna mafunzo ya stashahada hadi shahada nawasisitizia msisahau mafunzo ya muda mfupi mfupi kwa maana wakati huu wa Tanzania ya viwanda hayo ni muhimu tena sana” alisisitiza Majaliwa.

Alitoa mfano wa Chuo Kikuu Huria namna ambavyo kimesaidia kuinua elimu ambapo mwaka 1994 kilivyoanza huku serikali ikiwa na vyuo vikuu viwili kikiwepo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUA), Chuo hicho huria kilikuwa na wanafunzi 4175.

Aliongeza kutokana na thamani ya elimu ya watu wazima ambayo serikali imeweka, kwa hadi mwaka wa fedha 2019/2020

kimeshahudumia wahitimu 160,509 ambapo waliohitimu Shahada ni 70,423, Shahada ya Uzamili ni 37189 na Stashahada pamoja na Cheti 52,879.

Join our Newsletter